Cheki kufukuza makocha kulivyowakosti Man United

Muktasari:

Man United ilithibitisha Alhamisi iliyopita kwamba kumwondoa Mourinho na benchi lake la ufundi kumewagharimu Pauni 19.6 milioni.

Manchester, England. MANCHESTER United wanakuna kichwa kwa sasa. Wasikosee tena kwenye kuchagua kocha wa kudumu kwenye kikosi chao.
Unajua kwanini, kufanya hivyo kumewagharimu sana. Katika kipindi cha miaka sita tangu walipoachana na Sir Alex Ferguson, Man United imejikuta ikiingia hasara kwa kutumia Pauni 33.2 milioni kulipa makocha iliyowafukuza baada ya kuwapa kazi na kushindwa kuifanya vyema.
Katika kipindi hicho cha miaka sita Man United imeajiri makubwa wakudumu mara tatu na kuwafuta kazi wote. David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho wote wameshindwa kuvaa viatu vya Ferguson ipasavyo tangu alipoondoka kwenye kikosi hicho baada ya kudumu kwa miaka 26 na kuachia ngazi 2013.
Man United ilithibitisha Alhamisi iliyopita kwamba kumwondoa Mourinho na benchi lake la ufundi kumewagharimu Pauni 19.6 milioni.
Kocha Mourinho peke yake, ambaye aliipa klabu hiyo ya Man United ubingwa wa Kombe la Ligi na Europa League, ameweka mfukoni Pauni 15 milioni kwa kufutwa kazi huko Old Trafford. Walikuwa kwenye benchi lake, kocha wa makipa Silvino Louro, skauti wa kwenda kuwasoma wapinzani, Ricardo Formosinho, makocha wa viungo Stefano Rapetti na Carlos Lalin na mchambuzi wa mbinu na staili, Giovanni Cera walilipwa mgawo wa Pauni 4.6 milioni wagawane.
Mwaka 2014, kocha David Moyes na benchi lake la ufundi alipoondoka kwenye klabu hiyo baada ya miezi tisa katika mkataba wake wa miaka sita, ameigharimu timu hiyo Pauni 5.2 milioni alizolipwa kwa mkataba wake kuvunjwa.
Miaka miwili baada ya kumfuta kazi Moyes, Man United ilimfuta kazi kocha mwingine, Louis van Gaal.

Kocha huyo Mdachi alipoondolewa Old Trafford yeye na benchi lake la ufundi liliigharimu timu hiyo Pauni 8.4 milioni.

Baada ya hapo akaja, Mourinho, ambaye na benchi lake la ufundi limeigharimu timu hiyo pesa nyingi zaidi, karibu Pauni 20 milioni, huku robo tatu ya pesa hiyo ikienda kwenye mfuko wa kocha huyo Mreno.

Man United kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya wa kudumu, huku Mauricio Pochettino akipewa nafasi kubwa ya kupewa kibarua hicho mbele ya kocha wa sasa wa muda Ole Gunnar Solskjaer, ambaye mambo yake yamewafanya baadhi ya mabosi kwenye klabu hiyo ya Old Trafford kuamini kwamba anafaa kuchukua mikoba ya kudumu ya kuinoa klabu hiyo yenye hadhi kubwa England na duniani kote kwa ujumla.