WATU KIMYAAAAA! Mnyama anguruma Taifa

Muktasari:

Ushindi huo umeifanya Simba sasa kufikia mechi ya 31 ikishinda dhidi ya 36 za Yanga tangu mwaka 1965, huku mechi 35 zikiisha kwa sare

Dar es Salaam.Huko Msimbazi shangwe kama lote unaambiwa. Hii ni baada ya chama lao la Simba kuizima Yanga, katika mechi yao ya 102 katika Ligi ya Bara tangu zianze kukutana mwaka 1965.
Meddie Kagere MK14, ndiye aliyeamua pambano hilo baada ya kufunga bao pekee na la ushindi kwa Simba wakati wakiicharaza Yanga bao 1-0 katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.
Hicho kilikuwa kipigo cha pili kwa Yanga msimu huu, japo kimewaacha kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 58 baada ya mechi 24, huku Simba ikikwea kutoka nafasi ya tano hadi ya tatu kwa kufikisha pointi 39 kutokana na mechi 16 ilizocheza mpaka sasa.
Katika mchezo huo uliochezeshwa vyema na mwamuzi Hans Mabena kutoka Tanga, Simba ilionekana kutawala vipindi vyote, huku wakifanya mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani wao, ingawa hayakuwa na madhara hadi dakika ya 71, Kagere alipofunga bao hilo pekee.
Kagere aliyefikisha bao la tisa msimu huu katika ligi, alifunga kwa kichwa chepesi akiwa mbele ya mabeki Paul Godfrey na Abdallah Shaibu 'Ninja' sambamba na kipa wao, Ramadhani Kabwili aliyeandikisha rekodi jana kwa kucheza derby akiwa na umri wa miaka 18 na miezi miwili na siku tano. Kipa huyo wa timu ya taifa ya vijana U20, amezaliwa Desemba 11, 2000 na jana alijitahidi kuibeba Yanga huku akilindwa na ukuta wa chuma wa kina Kelvin Yondani, Andrew Vincent Dante na Ninja, huku pembeni kukiwa na Paul Godfrey 'Boxer' na Gadiel Michael.
Hata hivyo Kagere alimtibulia kwa kufunga bao hilo lililokuwa la 22 kwa straika huyo tangu aanze kuichezea Simba katika mechi za mashindano mbalimbali, yakiwamo sita ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

MCHEZO ULIVYOKUWA
Tofauti na mchezo wa kwanza ambao Yanga walionekana wazi waliingia kwa lengo la kujilinda, jana ilikuwa tofauti na walionekana wanataka kupata ushindi ili wazidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mchezo ulianza kwa Simba kutawala mpira na kufanya shambulizi la mapema langoni mwa Yanga kupitia upande wa kulia lakini Emmanuel Okwi aliunganisha vibaya kwa kichwa krosi ya Zana Coulibaly na kupaisha mpira huo.
Yanga ambao walikuwa wanatumia staili ya kupiga pasi ndefu, walijibu kwa kufanya mashambulizi mawili ambayo kama wangekuwa makini yangewaweza kuwapatia bao.
Shambulizi la kwanza lilikuwa la dakika ya nne ambapo mpira Yanga walipata faulo iliyochongwa vyema na Gadiel Michael na kutua kichwani mwa Amissi Tambwe lakini kipa Aishi Manula aliuwahi mpira wa kichwa wa mshambuliaji huyo.
Dakika tatu baadaye Yanga walifanya tena shambulizi la kushtukiza langoni mwa Simba lakini wapinzani wao walizima shambulizi hilo kwa beki Juuko Murshid kumchezea rafu Heritier Makambo lakini faulo hiyo hawakuweza kuitumia vizuri.
Baada ya mashambulizi hayo ya kushtukiza ya Yanga, timu hizo zilianza kushambuliana kwa zamu huku zikikosa nafasi kadhaa za hapa na pale ingawa Simba ndio walionekana kumiliki mpira katika dakika 30 za mwanzoni, wakipiga pasi fupifupi kuelekea langoni mwa wapinzani wao.
Simba walionekana kupatumia zaidi upande wao wa kulia ambao ulionekana kuwa tishio kwa Yanga kutokana na namna ulivyokuwa unatumika kupeleka krosi za mara kwa mara.
Beki wa kulia wa Simba, Zana Coulibaly ambaye anasifika kutokana na mbwembwe zake, alionekana kucheza kwa uhuru mkubwa kutokana na winga ya kushoto ya Yanga kushindwa kumpa changamoto.
Hata hivyo katika robo ya mwisho ya kipindi cha kwanza, Yanga waliamka na kuanza kumiliki mpira, wakitumia vyema udhaifu wa viungo wa Simba hasa Jonas Mkude na Cletous Chama ambao walipoteza pasi nyingi walizokuwa wakipiga eneo la katikati mwa uwanja.
Mabadiliko hayo ya kiuchezaji kwa Yanga kwenye kipindi hicho cha kwanza yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na kitendo cha nahodha Ibrahim Ajibu kuhamia pembeni huku kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' kuingia kucheza kama kiungo wa ndani.
Katika kipindi hicho cha kwanza, mashabiki wa timu zote mbili walimtupia lawama za hapa na pale mwamuzi Hans Mabena hasa pale alipokuwa akitoa maamuzi ambayo yalinufaisha upande wa pili.
Katika kipindi hicho cha kwanza, wachezaji Mohammed Hussein 'Tshabalala' wa Simba na Amissi Tambwe walijikuta wakionyeshwa kadi za njano na refa Mabena kutokana na utovu wa nidhamu.
Tshabalala alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Paul Godfrey 'Boxer' wakati Tambwe alipewa kadi kwa kosa la kushika mpira makusudi alipokuwa anataka kuunganisha krosi ya Ibrahim Ajibu.

KIPINDI CHA PILI
Taswira ya mchezo ilibadilika kipindi cha pili ambacho Simba ilikitawala vyema kuanzia mwanzoni hadi mwishoni, ikitawala mchezo na kutowapa nafasi Yanga ya kutopumua.
Hiyo ilikuwa ni baada ya Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa Cletous Chama aliyeonekana kuchemka kwenye mchezo wa jana kulinganisha na mechi nyingine za timu hiyo.
Nafasi ya Chama ilichukuliwa na kiungo Hassan Dilunga ambaye alibadilisha mchezo kwa kuiunganisha vyema timu, kwa kupiga idadi kubwa ya pasi za kwenda mbele ambazo ziliwafikia walengwa kwa usahihi.
Kwa upande wa Yanga walimfanyia mabadiliko Amissi Tambwe na nafasi yake kuchukuliwa na winga Mrisho Ngassa ikionekana ni mpango wa kupunguza nguvu ya Simba upande wa kulia.
Ubora wa Dilunga ulionekana mwiba kwa safu ya kiungo ya Yanga ambayo licha ya kumuingia kiungo Mohammed Issah 'Banka' ilishindwa kuwazima Simba ambao walitaka na kutengeneza nafasi kila wakati jambo lililoiweka Yanga kwenye hatari ya kuruhusu bao.
Na hicho ndicho kilikuja kutokea kwani mshambuliaji tishio kwenye kikosi cha Simba, Meddie Kagere alifanya kile kilichoonekana kinakuja kutokea baada ya kuipatia timu yake bao lililoipa ushindi kwenye mchezo huo muhimu.
Kagere alifunga bao hilo mnamo dakika ya 71 akiunganisha vyema kwa kichwa krosi kutokea upande wa kulia iliyopigwa na nahodha John Bocco.
Bocco kabla ya kupiga krosi hiyo alifanya kazi ya ziada kwa kumtoka mlinzi Gadiel Michael aliyeonyesha kiwango cha chini kwenye mchezo wa jana na kupiga krosi iliyotua kichwani mwa Kagere na kujaa wavuni huku kipa Ramadhan Kabwili akiwa hana la kufanya.
Baada ya kuingia bao hilo, Simba waliendelea kulisakama lango la Yanga kama nyuki wakitengeneza nafasi nyingi za mabao ambazo walishindwa kuzitumia vyema.
Safu ya ulinzi ya Yanga ilionekana kuchanganywa na bao hilo huku mabeki wake wakipaniki na kupelekea kufanya faulo ambazo zilisababisha Kelvin Yondani, Feisal Salum na Abdallah Shaibu kuonyeshwa kadi za njano.
Upande wa Simba kwenye kipindi cha pili wachezaji wake Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Juuko Murshid nao walionyeshwa kadi za njano kwa mchezo usio wa kiungwana.
Benchi la ufundi la Yanga liliwatoa Gadiel na Ibrahim Ajibu na kuwaingiza Mohammed Issah na Mateo Anthony ambao hta hivyo hawakuipa ufanisi timu.
Kwa upande wa Simba, mbali na Chama, pia waliwatoa Meddie Kagere na Emmanuel Okwi huku nafasi zao zikichukuliwa na Mzamiru Yassin na Haruna Niyonzima.

YANGA MCHECHETO
Kabla ya kuanza kwa mchezo huo, Yanga ilionekana kuwa na mchecheto kwa kuamua kutanguliza basi lao kubwa tupu na kutumia Toyota Coaster, huku pia wakigomea vyumba cvya kubadilishia nguo.
Wakiwa na uzi mopya kabisa kwenye mchezo huo wenye rangi za njano na ufito mpana wa kijani kifuani sambamba, Yanga waliingia uwanjani wakitumia sehemu isiyo rasmi watoto wa mjini huwa wanasema kuchepuka.
Yanga ambao ni wenyeji wa mchezo wa marudio wa Ligi Kuu Bara wa Simba na Yanga uliopigwa Uwanja wa Taifa.
Wakati wa kuingia timu hizo mbili uwanjani, wachezaji wa Simba upande wa kulia na wa Yanga kushoto.
Wao hawakupita katika eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya kuingia,  walipita kwa nje na kuwaacha wa Simba pamoja na wale viongozi wa mchezo huo wakipita sehemu hiyo.
Matukio kama haya huwa yanafanyika katika mechi za namna hii pindi timu pinzani za watani wa

DIDA VITUKO
Naye kipa namba mbili wa Simba,  Deogratius Munishi 'Dida' alifanya uamuzi magumu katika mchezo wao na Yanga wakati wanaingia uwanjani kwa ajili ya kipute hicho, mashabiki wa Yanga walimwita Dida na kumshangilia na yeye ikabidi awape salamu kwa kuwanyooshea mikono juu, jambo ambalo ni gumu kufanywa na wachezaji wakati wapinzani hao wanapokutana.
Hii  ni kutokana na ushindani uliopo Kwa timu hizo kongwe na pinzani nchini Tanzania.
Awali,  Dida aliwahi kuichezea Yanga kwa mafanikio miaka ya nyuma kabla ya kurudi na kujiunga na Simba kwa mara nyingine.

TAKWIMU ZILIVYOKUWA
Katika mchezo huo Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 60 dhidi ya 40 za watani zao, huku wakipata kona nne dhidi ya mbili za Yanga, huku vijana hao wa Msimbazi wakicheza faulo 19 dhidi ya 15 za Yanga, huku ikipiga jumla ya mashuti 14, matatu yakilenga lango na 11 yakienda nje.
Yanga wenyewe walipiga mashuti sita tu, moja likilenga lango la Simba na mengine matano yakipotea maboya, huku ikiotea mara mbili dhidi ya moja ya Simba na kupata kadi nne za njano dhidi ya tatu za watani zao.
Ushindi huo umeifanya Simba sasa kufikia mechi ya 31 ikishinda dhidi ya 36 za Yanga tangu mwaka 1965, huku mechi 35 zikiisha kwa sare na bao la Kagere limeifanya Simba ifikishe mabao 97 dhidi ya 107 ya Vijana wa Jangwani.

REKODI ZIMESHINDWA KUVUNJWA
Licha ya Kagere kuingia kwenye orodha ya nyota wa Simba walioitungua Yanga, lakini mechi ya jana imeshindwa kuvunja rekodi kibao zilizowekwa kwenye mechi za watani ikiwamo ya hat trick inayoshikiliwa na Abdallah Kibadeni aliyefanya hivyo Julai 19, 1977 wakati Simba ikishinda 6-0.
Rekodi nyingine iliyoshindwa kuvunjwa ni ile ya mfungaji wa muda wote inayoshikiliwa na Omary Hussein aliyekuwa akiichezea Yanga aliyefunga mabao sita, sambamba na kushuhudia Yanga ikishindwa pia kulipa kisasi cha mabao 6-0 ilichopewa karibu miaka 42 iliyopita.