Aussems alivyomzidi ujanja Zahera, Simba shangwe

Muktasari:

Mshambuliaji Kagere amefunga bao lake la kwanza katika mchezo wa watani wa jadi

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wamefanya kile kilichotarajiwa na mashabiki wao baada ya kuichapa Yanga kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shujaa wa Simba katika mchezo huo alikuwa na mshambuliaji Meddie Kagere aliyefunga bao pekee la Simba katika dakika 71, akimaliza kwa kichwa krosi ya nahodha John Bocco.

Kagere amefunga bao lake la tisa katika Ligi Kuu na kuisaidia Simba kufikisha pointi 39, katika nafasi ya tatu wakati Yanga ikibaki kileleni na pointi 58.

Katika mchezo huo kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alianza kwa kucheza kwa kulinda zaidi kwa mfumo wa 4-1-3-2 na kumwacha Heritier Makambo akiwa mshambuliaji pekee.

Wakati kocha wa Simba, Partick Aussems akiingia na mfumo wake wa 4-4-2, uliwafanya kutawala zaidi eneo la katikati ya uwanja, lakini pasi zao nyingi zilikuwa hazina madhara langoni mwa Yanga.

Katika mchezo huo hadi timu hizo zinakwenda mapumziko si Yanga wala Simba ambayo mashuti yao yalikuwa yamelenga goli.

Simba ilipiga mashuti manne yaliyotoka nje wakati Yanga ilikuwa imepiga mashuti mawili yalishoshindwa kulenga goli kadi mapumziko.

Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko kwa lengo kutawala mchezo Yanga ilimtoa Ajib na Tambwe na kuwaingia Mrisho Ngasa na Mohamed Issa ‘Mo Banka’ wakati Simba iliwaingiza Hassan Dilunga kuchukua nafasi ya Chama.

Simba ilifaidika na kuingia kwa Dilunga aliyeongeza mashambuliaji ya kasi wakati Mo Banka na Ngassa walishindwa kuisaidia Yanga katika safu ya kiungo.

 CHAMA APOTEZWA

Kiungo Clatous Chama alishindwa kabisa kutamba katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, kiasi cha kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga.

Ipo hivyo katika mchezo unaoendelea katika Uwanja wa Taifa katika eneo la katikati kumewaka kinoma.

Eneo hilo la kiungo limekutana na changamoto kubwa kutokana na viungo wote kila mmoja kutaka kufanya kazi yake kiufasaha.

Simba katika eneo la kiungo waliwaweka Chama, Jonas Mkude na James Kotei, huku Yanga wakiwaweka Feisal Salum, Abdallah Shaibu na Papy Tshishimbi.

Viungo wa Simba walionekana zaidi kucheza katika eneo hilo, lakini viungo wa Yanga waliweza kukaba zaidi na kuhakikisha hawapitwi katika eneo hilo.

Chama alizoeleka kupita ngome ngumu, alishindwa kabisa kutawala na kufanya makubwa katika mchezo huu baada ya kuwa chini ya ulinzi wa Abdallah Shaibu ' Ninja'

Kitendo hicho kilimfanya kocha Patrick Aussems kufanya mabadiliko dakika 45 kwa kumtoa Chama na nafasi yake ilichukuliwa na Hassan Dilunga.

Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Amis Tambwe, Ajibu na kuwaingia Mrisho Ngassa na Mohammed Issa ‘Mo Banka’.

UPWEKE WAMTESA MAKAMBO

Kitendo cha kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kumchezesha Heritier Makambo kama mshambuliaji pekee kuliwafanya mabeki wa Simba wasiwe na kazi kubwa ya kufanya.

Mabeki wa Simba wakiongozwa Pascal Wawa na Juuko Murshid walikuwa makini kumdhibiti Makambo ambaye hakuonekana kabisa kufurukuta ndani ya dakika 45.

Licha ya Amis Tambwe kuwepo katika eneo la ushambuliaji, hakuweza kusimama zaidi katika eneo la ushambuliaji badala yake alikuwa akitokea katikati na kusogea juu kitu ambacho kiliwapa nguvu Simba kuzuia bila wasiwasi.

Hata hivyo Yanga waliamua kutumia mipira ya pembeni kupitia kwa Paul Godfrey kupeleka mashambulizi, lakini bado krosi ambazo zilikuwa zinapigwa hazikuweza kuzaa bao lolote.

Simba wao katika eneo la ushambuliaji walianzisha washambuliaji wawili na walionekana zaidi kushambulia mfululizo katika goli la Yanga, hata hivyo hawakuweza kupata bao ndani ya dakika 45.

MASHABIKI WAZIMIA

Baada ya Simba kupata bao kupitia kwa Meddie Kagere mashabiki wawili wa Simba wanawake walizimia.

Mashabiki hao walikuwa wamekaa katikati ya wenzao wa Simba, walidondoka na ndipo zikasikika kelele za kuitwa kikosi cha uokoaji.

Hata hivyo, kikosi cha uokoaji kilifika eneo hilo na kuwatoa katikati ya umati na kuwapeleka katika vyumba vya matibabu.

Kikosi hiko cha uokoaji kilizidi kupitisha macho katika majukwaa ya mashabiki kuona kama kuna shabiki mwingine amepatwa na matatizo.

Hii imekuwa ni kawaida kwa mashabiki kuzimia pindi timu hizi za Simba na Yanga zinapokutana katika michezo yao.

BEKI YANGA APAGAWISHA

Beki wa Yanga, Paul Godfrey amegeuka nyota kwa kushangiliwa na mashabiki wa klabu hiyo.

Godfrey katika mchezo huu alikuwa ndio muhimili katika kupeleka mashambulizi ya haraka kutokana na kasi yake ya kutosha kuvuka na kuingia katika upande wa Simba.

Beki Mohammed Hussein wa Simba, alijikuta akiwa katika kazi ya ziada kumzuia Godfrey, kiasi kilichomfanya ashindwe kabisa kupanda kama ilivyozoeleka.

Hali hiyo ilisababisha Simba wamtumie zaidi Zana Coulibaly katika kupeleka mashambulizi kuliko Tshabalala.

Godfrey ni mchezaji chipukizi aliyepewa nafasi ya kucheza na mwalimu Mwinyi Zahera katika kikosi cha kwanza.

VIKOSI

Yanga: Ramadhan Kabwili, Paul Godfrey, Gadiel Michael, Andrew Vicent, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu, Feisal Salum, Papy Tshishimbi, Herieter Makambo, Amis Tambwe na Ibrahim Ajib.

Simba: Aish Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.