Marefa hawa walivulunda mechi za watani jadi

Muktasari:

Mechi baina ya watani wa jadi imekuwa na idadi kubwa ya matukio ya ndani na nje ya uwanja ambayo yanaweza kuwa kumjengea sifa mwamuzi ama kumpoteza kutegemeana na jinsi atakavyochezesha.

Dar es Salaam. Mwamuzi Hans Mabena kutoka Tanga ndiye atakayeshika filimbi kwenye pambano la Watani wa Jadi, Yanga na Simba leo Jumamoisi kwenye Uwanja wa Taifa.
Hii ni mechi ya kwanza kubwa kwa Mabena kuchezesha kwani kabla ya hapo hakuwahi kufanya hivyo kwenye hata pia zile mechi zinazokutanisha Yanga au Simba dhidi ya Azam FC.
Mechi baina ya watani wa jadi imekuwa na idadi kubwa ya matukio ya ndani na nje ya uwanja ambayo yanaweza kuwa kumjengea sifa mwamuzi ama kumpoteza kutegemeana na jinsi atakavyochezesha.
Wapo waamuzi waliowahi kung'aa kwenye mechi za watani lakini pia wapo waliowahi kuchemka au kuacha historia isiyo nzuri katika mchezo unaokutanisha timu hizo.
Makala hii inakuletea orodha ya baadhi ya marefa ambao walijikuta wakiwa kikaangoni kutokana na kushindwa kuhimili presha na matukio ya mechi za watani.

Martin Saanya
Mwamuzi Martin Saanya alikutana na upepo mbaya wa mechi ya Watani wa Jadi mwaka 2016 ambayo ilisababisha afungiwe kwa misimu miwili kwa kile kilichotafsriwa kuwa ni kushindwa kulimudu pambano hilo.
Kwenye mchezo  huo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, Saanya aliruhusu bao la Amissi Tambwe ambaye kabla ya kufunga aliushika mpira kwa mkono lakini pia alitoa kadi nyekundu kimakosa kwa aliyekuwa nahodha wa Simba, Jonas Mkude ambayo hata hivyo baadaye ilifutwa.
Lakini pia Saanya alikataa bao la mshambuliaji Ibrahim Ajibu ambaye wakati huo alikuwa anachezea Simba baada ya mwamuzi msaidizi, Samuel Mpenzu kuonyesha kibendera akiashiria kuwa mfungaji aliotea tofauti na uhalisia.
Kutokana na kukataliwa kwa bao hilo, Mpenzu naye alijikuta akifungiwa kwa kipindi cha misimu miwili.

Oden Mbaga
Mwaka 2011, presha ya mchezo wa Yanga na Simba ilimweka matatani mwamuzi mzoefu na miongoni mwa waliokuwa wanasifika kwa kutafsiri vyema sheria 17 za mchezo wa mpira wa miguu nchini, Oden Mbaga.
Katika mchezo huo uliochezwa Machi 5, Mbaga aliruhusu bao la kusawazisha la Simba lililofungwa na Musa Hassan 'Mgosi' kwa kutumia msaada wa luninga kubwa iliyokuwepo uwanjani ambayo ilionyesha marudio ya bao hilo ambalo refa huyo alichelewa kulikubali au kulikataa.
Shuti hilo la Mgosi, liligonga mwamba wa juu na kudondokea nyavuni lakini wachezaji wa Yanga waliwahi kuuondosha mpira huo jambo lililomchanganya Mbaga na msaidizi wake ingawa baadaye kwa msaada wa luninga waliamuru kuwa ni bao halali. Hata hivyo kanuni za ligi ya Tanzania haziruhusu matumizi ya luninga katika kuwasaidia waamuzi.

Omar Abdulkadri
Refa Omar Abdulkadir naye alikumbana na jinamizi la mechi ya Watani wa Jadi mwaka 2002 ambapo uamuzi wake wa kuruhusu bao la mshambuliaji wa Simba, Madaraka Selemani ambaye aliutuliza mpira kwa mkono kabla hajafunga nusura usababishe chezo wa fainali ya Kombe la Tusker baina ya timu hizo uvunjike.
Mara baada ya kukubali bao hilo, umati wa mashabiki wa Yanga ulifanya vurugu kubwa kwa kurusha vitu uwanjani na kwenye jukwaa kuu huku timu hiyo ikitaka kugomea mchezo ingawa baadaye hali ilitulia na mchezo kumalizika huku Simba ikishinda mabao 4-1.

Mathew Akrama
Mwezi Oktoba mwaka 2012, Mwamuzi Mathew Akrama naye alisombwa na mafuriko ya mechi za watani wa jadi baada ya kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kutokana na makosa aliyoyafanya ya kutomudu mchezo na kushindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka.