Kila kona ni Makambo, Kagere hapatoshi

Muktasari:

Makambo na Kagere pamoja na mafanikio bado hawajafunga mabao katika mechi ya watani wa jadi Yanga, Simba

Dar es Salaam. Wakati mpambano wa watani wa jadi Yanga na Simba ukitarajia kufanyika keshokutwa, kivutio kikubwa katika mchezo huo kitakuwa kwa washambuliaji wawili Heritier Makambo na Meddie Kagere.

Wachezaji hao wamekuwa kivutio kwa mashabiki wa klabu hizo mbili na kila mmoja anaongoza kwa ufungaji katika kikosi chake kwenye Ligi Kuu Bara.

Makambo anayeongoza katika msimamo wafungaji akiwa amefunga mabao 11 wakati Kagere anashika nafasi ya sita akiwa amefunga mabao manane lakini anawaburuza kwa ufungaji wachezaji wenzake kwenye klabu yake. 

Makambo amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga licha ya kwamba hakuwa katika kiwango bora katika mechi tatu za hivi karibuni kiasi cha kocha wake Mwinyi Zahera kumuonya na kumtaka kurejesha ubora wake.

Hata hivyo mchezaji huyo anaweza kuibuka katika mechi ya keshokutwa na kufunga bao na kuwanyamazisha mashabiki wa Simba ambao wanaamini hatafurukuta mbele ya mabeki wao Pascal Wawa, Juuko Murshid na Yusuph Mlipili.

Pia mabeki wa Yanga wakiongozwa na Kelvin Yondani 'Vidic', Andrew Vincent 'Dante'na Abdallah Shaibu 'Ninja' watakuwa na kazi kubwa ya kumbana Kagere asifunge kwani ameonekana hivi sasa yuko katika kiwango kikubwa.

Kufunga bao katika mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly Jumanne iliyopita na kuipa timu yake ushindi kumemuongezea morali mchezaji huyo ambaye anatazamiwa kufanya makubwa katika mchezo wa Jumamosi.