Mbelgiji, Tambwe walianzisha mapema

Muktasari:

Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa, likiwa pambano lao la marudiano baada ya suluhu kwenye mchezo wa kwanza.

Dar es Salaam.Presha na joto la homa la pambano la watani, baada ya straika mwenye bahati ya kuitungua Simba, Amissi Tambwe kulianzisha mapema, huku Kocha wa Msimbazi, Patrick Aussems akisisitiza kwa sasa akili yake ipo kwa Waarabu kuliko Yanga aliamua kuwaotezea kimtindo.

Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa, likiwa pambano lao la marudiano baada ya suluhu kwenye mchezo wa kwanza, lakini Aussems alisema baada ya kumalizana na Mwadui walioinyuka mabao 3-0 akili zake amehamishia mechi yao ya Al Ahly.

Mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa itapigwa Jumanne na Mbelgiji alisema ndio inayomuumiza kichwa kuliko pambano la Yanga akidai akishamalizana na Waarabu ndio ataanza mikakati kuelekea pambano hilo alilodai analichukulia kama mapambano mengi ya ligi.

"Katika mechi na Mwadui tulikuwa na kipindi cha kwanza kizuri ambacho tuliweza kufunga mabao, lakini tulishindwa kumaliza mechi kwa kufunga zaidi kutokana katika vichwa vya wachezaji wangu kuna mawazo mengi zaidi ya mechi inayofuata na Al Ahly," alisema.

Alisema makosa yaliyojitokeza mbele ya Mwadui na hata kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya Al Ahly yamerekebishwa, ili kuwanyamazisha wapinzani wao, kisha ndipo aanze kuufikiria mchezo wao ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga.

"Tukimalizana na Al Ahly ndio tutaanza maandalizi ya mechi ya Yanga, kwani malengo yetu ni kuchukua pointi tatu katika mechi zetu zote za viporo, nashukuru tumeanza na Mwadui na kushinda sasa akili yetu inaenda kwa katika mechi ya Al Ahly lengo likiwa ni kushinda pia."

MSIKIE TAMBWE SASA

Upande wa Tambwe anayeshikilia rekodi ya kuitungia Simba mara tatu mfululizo kama ilivyo kwa Shiza Kichuya aliyetimkia Misri na mkongwe wa zamani wa Simba, Madaraka Seleman, alisema amerudi rasmi uwanjani na kwamba watani zao wajipange kwani lazima walie Taifa.

Tambwe aliumia kwenye mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Biashara United na kushonwa nyuzi tatu, huku timu yake ikipenya kwa penakti 5-4 baada ya sare ya 2-2 katika dakika 90.

Tambwe alisema Simba ina jina kubwa, lakini haina kikosi cha kuwazuia Yanga wasishinde mbele yao watakapokutana kwani safu yao ni nyepesi mno.

"Tumecheza nao duru la kwanza wakiwa na kikosi hicho hicho hicho kila mmoja aliondoka na pointi moja hawatutishi na ukizingatia wametoka kupata matokeo mabaya mfululizo katika Ligi ya Mabingwa, kilichowaangusha ni ukosefu wa nidhamu katika kwa mabeki wake," alisema.

"Tumeshafahamu mapungufu yao yako wapi na ubora wao uko wapi tutavitumia ili kupata alama, kwani mipango ya kuhakikisha tunarudi tena katika michuano ya Afrika," aliongeza.

Akizungumzia ari ya kikosi chao kwa sasa alisema kinazidi kuimarika japo kimekuwa kikikumbana na changamoto ya majeruhi kutokana na kucheza michezo mingi mfululizo na kuweka wazi bado hilo haliwezi kuwa sababu ya kupoteza mchezo wao ujao wikiendi hii.