Afrigo Bendi, Shams Music wang'arisha Sauti za Busara

Muktasari:

Bendi mbili kutoka Kenya na Uganda wameng'arisha tamasha la sauti za busara, kwa kutoa burudani kupitia ujumbe wa kauli mbiu ya tamasha hilo.

Zanzibar. Kama unaamini muziki wa dansi unayumba duniani utakuwa unakosema.

Hii imedhihirishwa na bendi mbili kubwa za muziki wa dansi kutoka Kenya, Shams na Uganda, Afrigo baada ya kung'arisha tamasha la Sauti za Busara 2019 kwa kutumia ubunifu wa kutaja kauli mbiu ya tamasha 'Potezea rushwa sio dili' kila baada ya wimbo kuisha jukwaani.

Kutokana na ushirikiano wa wasanii ndani ya bendi hizo, wameweza kulitawala jukwaa vema kupitia ujumbe huo huku wakiwaimbisha mashabiki na kuongea maneno ya kuashiria wadau wa muziki wa dansi wasikate tamaa kwa kufifia kwa muziki huo katika tamasha hili la 16 toka kuanzishwa.

Kwa upande wa Shams bendi kutoka Kenya walipanda jukwaani saa 3:00 usiku nakuanza kutoa burudani, ilipofika tatu na dakika arobaini na tano walisimamisha muziki na kuanza kuongelea rushwa inavyosababisha muziki wa dansi ushindwe kuyumba na kushindwa kurudi kwenye chati.

Huku Afrigo walipanda saa 5:00 kamili jukwaani, walitoa burudani huku wakichomokea maneno ya kusifia muziki wa dansi na kusema hakuna kukata tamaa kwani nafasi bado ipo ya kuweza kuurudisha muziki mahala pake na kuwaimbisha watu kauli mbiu ya Tamasha la Sauti za Busara kuwa potezea rushwa sio dili.

Wakizungumza na Mwananchi Digital  kwa nyakati tofauti kuhusu  ubunifu huo  Shams wamesema "wanashukuru Sauti za Busara kwa kuweka ujumbe kuhusu rushwa kwani, muziki wa dansi wa sasa umekuwa tofauti na zamani na hii ni kutokana na baadhi ya media kushindwa kutoa sapoti na kutaka rushwa, hivyo wameamua kuulilia jukwaani kwani bado inahitajika nguvu zaidi."

Kwa upande wa Afrigo "Kama mlivyoona mashabiki wamechangamka kwa sababu wanaelewa muziki wa dansi, hivyo kuzungumzia rushwa jukwaani ni pamoja na kuisukuma kauli mbiu iliyowekwa na wahusika wa tamasha la Sauti za Busara, na ukiangalia baadhi ya nchi nyingi muziki wa dansi umekuwa ukisua sua tofauti na zamani"