Fei Toto atupia, Yanga yaichapa JKT Tanzania

Muktasari:

Ushindi unaifanya Yanga kushindi mechi 18, kati 22 ilizocheza ikifungwa moja na kutoka sare 4 hadi sasa katika Ligi Kuu bara

Tanga. Bao la kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ limetosha kuipa Yanga ushindi mwembamba 1-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Fei Toto alifunga bao hilo pekee katika dakika 26, na kuifanya Yanga kujikita kileleni kwa pointi 58, huku Azam ikiwa ya pili pointi 48, na Simba ikiwa ya watatu 36.

Ushindi huo wa Yanga unawaweka katika mazingira mazuri kabla mechi ya watani wa jadi dhidi ya Simba itakayopigwa Februari 16, kwenye Uwanja wa Taifa.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema ushindi dhidi ya JKT Tanzania umezidi kuwaweka katika nafasi nzuri, lakini hakuwa akijua kama mechi hayo atacheza na Simba.

Mapema kikosi cha Yanga kilivyowasili katika uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga mchezaji wa kwanza kushuka katika gari ni kiungo Kabamba Tshishimbi.

Wachezaji wa Yanga kama kawaida yao walipofika uwanjani hapo hawakuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo kama walivyofanya katika mechi dhidi ya Coastal Union.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0, ambalo lilifungwa dakika 26, na kiungo Faisal baada ya kupokea pasi safi ya pembeni kutoka kwa beki wa kushoto Gadiel Michael.

Yanga ilifanya mabadiliko dakika 58 alitoka Mrisho Ngassa na kuingia Mohammed Issa 'MO Banka' ambaye anakitumikia kikosi cha Yanga tangu alipo maliza kuitumia azabu yake Februari 8, ya kukutwa na matumizi ya dawa aina ya bangi ambayo hazikubaliki michezoni.

Dakika 67, Yanga walifanya mabadiliko mengine walimtoa nahodha Ibrahim Ajibu na kuingiza Deus Kaseke, dakika tisa baadae walimtoa Buswita na kumuingiza Kelvin Yondan.

Dakika 76, JKT Tanzania walifanya mabadiliko alitoka Samwel Kamuntu na kuingia Said Luyaya.

Kocha wa JKT Tanzania, Bakari Shime alisema wachezaji wake hawakutumia vyema nafasi licha ya kucheza vizuri

Katika mchezo mwingine leo, Alliance imepanda nafasi ya saba baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na KMC kwenye Uwanja wa Uhuru.