Ishu ya viporo vya Simba kumbe ipo hivi buana!

Muktasari:

Kinachostaajabisha ni kwamba wakati Simba ikibebwa nchini kwa kisingizio cha ushiriki wa michuano hiyo ya CAF, wapinzani wao wa Kundi D, yaani Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo na JS Saoura ya Algeria zenyewe zimekuwa zikicheza mechi zao kama kawaida.

Dar es Salaam.Gumzo kubwa kwa sasa ni ishu ya viporo vya timu ya Simba katika Ligi Kuu Bara. Simba ilikuwa haijashuka uwanjani kwa siku 41 tangu walipokuwa wamecheza mchezo wa mwisho wa Ligi hiyo Desemba 29 walipovaana na Singida United na kushinda mabao 3-0.
Baada ya siku hizo, ndipo Alhamisi iliyopita ikarudi tena uwanjani kwenye ligi hiyo kwa kuvaana na Mwadui na kushinda pia mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo dhidi ya Mwadui ulikuwa ni wa 15 kwa Simba, huku Ligi Kuu ikiwa imeshaingia raundi ya 25, ikiwa na maana wakati wengine wakielekea kuifikia nusu ya duru la kwanza, Wekundu wa Msimbazi haijamaliza hata mechi zake za duru la kwanza.

Klabu hiyo imeandika rekodi ya kuwa klabu yenye viporo vingi katika ligi ya msimu mmoja na kuibua sintofahamu kwa wadau, wengi wakihisi kama kuna hila zinafanyika baina ya Simba na wasimamizi wa soka, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB).

Simba imejikuta na mechi sita karibia 10 za viporo kwa sababu ya ushiriki wake wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiiwakilisha nchi msimu huu.

Hata hivyo kitu kinachostaajabisha ni kwamba wakati Simba ikibebwa nchini kwa kisingizio cha ushiriki wa michuano hiyo ya CAF, wapinzani wao wa Kundi D, yaani Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo na JS Saoura ya Algeria zenyewe zimekuwa zikicheza mechi zao kama kawaida.

Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kuwa, klabu hizo wenza wa kundi la Simba zimekuwa zikicheza mechi za ligi zao za nyumbani kiasi kwamba hazitofautiani sana na wapinzani wenzao wa ligi hizo na inaelezwa huenda imechangia kuzifanya zitishe kundini kuliko Wekundu hao.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, tangu Simba ilipocheza mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu Desemba 29 mwaka jana dhidi ya Singida wapinzani wao wa Kundi D wamecheza zaidi ya mechi tano ambazo zinaelezwa zimechangia kuzifanya ziizidi Simba kwa kiasi kikubwa kundini.

Kocha Patrick Aussems ameanika ukweli wa wingi wa viporo hiyo, huku Bodi ya Ligi nayo kwa upande mmoja umeeleza kwanini wameiachia Simba kuwa na viporo vingine na kipi ambacho wanaenda kukifanya sasa ili kuondokana na aibu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

WAPINZANI WAO

JS Saoura(Algeria)

Huko Algeria JS Saoura inayoburuza mkia katika kundi D, lakini katika ligi ya kwao imeendelea kucheza mechi za ligi na itaendelea mpaka mwisho wa ratiba hiyo ya mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Takwimu zionaonyesha kuanzia Desemba 27 Saoura imecheza jumla ya mechi nne za ligi huku mechi za Ligi ya Mabingwa zikiwa tatu.

Katika mechi za ligi imepoteza mechi tatu dhidi ya Lakhdaria ugenini (1-0), kisha ikapoteza nyumbani dhidi ya JS Kabylie (0-1) na kulala tena mbele ya USM Alger ugenini kwa mabao 2-0 na kutoa sare moja ugenini dhidi ya Oran (1-1).

Ligi ya Mabingwa ikapokea kipigo dhidi ya Simba ugenini (0-3), kisha kutoa sare nyumbani dhidi ya Al Ahly (1-1) na baadaye ikalazimisha sare nyingine ugenini dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo (2-2).

Ratiba ya ligi ya kwao inaonyesha Saoura itacheza mechi zisizopungua sita za ligi mpaka kufikia mwisho wa ratiba ya mechi za hatua ya makundi huku pia ikibakiza mechi tatu katika ligi ya Mabingwa.

AS VITA CLUB

Upande wa AS Vita ya DR Congo ambao wanashika nafasi ya pili katika kundi hilo la Simba kuanzia Desemba 27 imeshacheza mechi saba za Ligi Kuu ya Kongo, ikishinda sita na kutoa sare moja.

Vita kati ya  Desemba 27 mwaka jana imecheza mechi dhidi ya Sanga Balende ugenini na kushinda 1-0, Don Bosco (4-2), Lubumbashi Sport (3-0) kabla ya kurudi nyumbani Kinshasa na kuzifunga Motema Pembe (3-1), Groupe Banzano (2-0) na Don Bosco (4-1), huku akitoa suluhu moja Groupe Banzano ugenini (0-0).

Ratiba inaonyesha juzi Vita Club alishinda ugenini AC Rangers (1-2) ambapo mechi zingine zijazo za ligi zitamkutanisha na Sanga Balende nyumbani, AS Maniema na TP Mazembe zote nyumbani kisha akitakiwa kusafiri ugenini kuwafuata St Eloi Lupopo.

Hata hivyo AS Vita imekuwa ikicheza mechi za Ligi ya Mabingwa ambapo huko imeshinda moja dhidi ya Simba nyumbani kwa ushindi wa mabao (5-0), kisha kuchapwa ugenini dhidi ya Al Ahly (2-0) na baadaye kutoa sare nyumbani dhidi ya JS Saoura ya (2-2).

AL AHLY

Vinara wa kundi D Al Ahly nao wamekuwa wakiendelea na ligi wakicheza mechi tano za ligi kuanzia Desemba 29 mwaka jana wakishinda wakishinda tatu na kutoa sare moja na kupoteza moja.

Ahly imezichapa ugenini Misr Elmaqasah (3-0), Wadi Degla (2-1), Smouha (1-0) kisha kutoa sare ugenini ya mabao (2-2) dhidi ya El Daldayeh na kuchapwa ugenini dhidi ya Pyramid (2-1). Mara

Ikiwa katika Ligi ya Mabingwa Ahly imeshinda mechi mbili nyumbani dhidi ya AS Vita (2-0) na Simba (5-0) na kutoa sare moja ugenini dhidi ya JS Saoura (1-1). Mara baada ya kuifumua Simba 5-0, iliwafuata ENPPI anayoichezea Shiza Kichuya na kushinda mabao 2-1.

Hata hivyo ratiba yao ya ligi Alhy itaendelea kucheza ligi mpaka kumaliza mechi za makundi ikitakiwa kukutanana na Haras El Hodood, El Masry nyumbani kisha kuwafuata ugenini El-Entag El-Harby.

WASIKIE TPBL

Kelele za wingi wa viporo vya mechi za Simba, vimemfanya Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura kufafanua baada ya kuulizwa kulikoni, Simba haichezi mechi wakati wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakati mechi hizo za ligi zingewasaidia.

Wambura alisema Simba kutocheza mechi zake kumetokana na ratiba ya mashindano tofauti ya Kombe la Mapinduzi na michuano ya mdhamini mkuu wa klabu hiyo Sportpesa.

"Unajua hili suala la mashindano ya Kombe la Mapinduzi na michuano ya Sportpesa ndio iliyovuruga ratiba hii ukiangalia hizo klabu unazosema hazikuwa na mashindano mengine," alisema Wambura.

Wambura alifafanua maamuzi ya Simba kutocheza mechi zake hayakutokana na maombi yao bali yalitokana na suala hilo, huku pia changamoto ya viwanja ikichangia kwa wamiliki kuwa na wa viwanja kuwa na shughuli wakati Simba ikitakiwa kucheza mechi zake.

"Sio kwamba Simba waliomba kutocheza hizo mechi ni kutokana na hizo changamoto, pia jingine ni viwanja Simba haina uwanja wake sasa kuna wakati tuliwapangia kucheza mechi Desemba 31 Uwanja wa Taifa lakini wenye uwanja wakasema uwanja umeshapata kazi nyingine katika siku hiyo."

Hata hivyo Wambura alisema baada ya changamoto hiyo ratiba ya viporo hivyo imeshapangwa na kwamba Simba atacheza mechi zake zote za viporo zitakazotakiwa kumalizika kabla ya kufikia raundi 10 za mwisho za ligi.

"Tumeshapanga hiyo ratiba ya hivyo viporo sio Simba tu klabu zote ambazo zina viporo tunataka mechi zao zichezwe kabla ya kufikia raundi kumi za mwisho na Simba atyacheza mechi zake hizo nyingi pale wakati mashindano ya Afcon ya vijana hasa zile za uigenini."

Kabla ya hapo Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto alieleza viporo vya Simba vilichangiwa zaiidi na wao wenyewe kuomba kila mara kuahirishiwa mechi zao ili kujiandaa na michuano ya Ligi ya CAF.

"Tatizo limechangiwa zaidi na Simba, wamekuwa wakiomba mechi zao ziahirishwe ili wapate muda wa maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa, lakini kwa sasa lazima watacheza mechi zao kwao ligi inatakiwa kumalizika kwa wakati," alisema Mnguto na kuongeza;

"Kwa msimu ujao haya mambo hayatakuwepo tena, kwani hata mimi yananipa wakati mgumu pamoja na wenzangu, lakini hatuna jinsi yameshatokea na sasa tunahakikisha kila kitu kinaenda kilivyopangwa."

AUSSEMS HUYU HAPA

Msikie Kocha Patrick Aussems anavyozungumzia viporo hivyo, kwani  alisema tangu kuanza kwa msimu huu amewahi kuomba mara moja tu kuahirishwa kwa mechi moja ya ligi  na mchezo huo ulikuwa karibu na mechi muhimu ya kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

"Unajua mkataba wangu una mambo makubwa mawili kwanza ni kuhakikisha timu inafuzu hatua ya makundi Afrika ambayo tumeshaifikia lakini pili ni kutetea ubingwa wa ligi kuu nakumbuka niliwahi kuomba mechi moja kusogezwa mbele ya ligi wakati tunatafuta tiketi ya kushiriki hatua ya makundi," alisema Aussems.

Mbelgiji huyo alisema katika mechi zilizofuata hakuwahi kuomba kuahirishwa kwa mechi hizo kutokana na mechi za ligi ni muhimu kuhakikisha anatimiza malengo ya klabu yake.

"Sijawahi kuomba mechi yoyote nyingine ziahirishwe ukiacha mchezo niliokuambiwa wakati tunajiandaa kurudiana na Nkana Red Devils. Nafahamu sasa nina kazi kubwa ya kuhakikisha Simba inatetea ubingwa wake na hilo litatimia kwa kucheza mechi."

Alisema sasa klabu yake itakuwa na ratiba ngumu katika mechi hizo zitazopangana karibu na kwamba wasiwasi wake ni mechi ambazo Simba itakiwa kusafiri kwenda ugenini mbali hatua ambayo inaweza kuwachosha wachezaji wake.

"Naona sasa tunaweza kuwa na ratiba ngumu sana ya kucheza mechi hizi kwa ukaribu na wasiwasi wangu mkubwa ni zile mechi za mbali ambazo tunaweza kuja kwachosha wachezaji kwa safari ndefu."