Samagol ameshindikana Ulaya

Muktasari:

Samatta anaongoza katika orodha ya wafungaji akiwa amefunga mabao 19, akifuatiwa na Hamdi Harbaoui wa Waregem mwenye mabao 14 na Landry Dimata wa Anderlecht mwenye mabao 13

Dar es Salaam. Ameshindikana. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Straika wa kimataifa na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ kujiwekea rekodi ya kumtesa kipa wa kutegemewa wa timu ya taifa ya Mexico, Guillermo Ochoa.

Samagoal akiwa na KRC Genk, juzi Ijumaa kwenye Uwanja wao wa nyumbani, Luminus alimtungua mara mbili Ochoa anayeidakia Standard Liège katika mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’.

Mchezo huo, ulikuwa ni watatu kwa Samagoal kukutana na Ochoa, mmoja wa makipa bora katika Ligi ya Ubelgiji huku  akibebwa na kuiongoza kwake msimu uliopita Standard Liège  kutwaa kombe la FA nchini humo.

Pia kipa huyo wa Fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Mexico kilichotwaa taji hilo Fainali za Kombe la Mataifa ya Amerika Kaskazini, CONCACAF Gold kwenye miaka ya 2009, 2011 na 2015.

Ndani ya michezo hiyo mitatu, Samagoal mwenye miaka 26 amejiwekea heshima mbele ya kipa hiyo kwa kuwa na wastani wa kufunga kwenye kila mchezo pindi akiwa golini.

Ochoa alijiunga na Standard Liège 2017 akitokea Malaga ambao akiwa huko alikutana na Samagoal kwa mara ya kwanza, Agosti 4 ndani ya mwaka huo, KRC Genk ilipoteza kwa mabao 2-1.

Katika mchezo huo, Samatta hakufunga, nahodha huyo wa Taifa Stars alianza kufungua akaunti yake ya mabao kwa Ochoa, Oktoba 28 mwaka jana kwenye sare ya 1-1.

Mchezo wa Jumamosi ambao Samagoal alifunga mara mbili mbele ya Ochoa umemfanya  kufikisha  mabao matatu dhidi ya kipa huyo.

WAMUACHIE KIATU MAPEMA

Kasi ya ufungaji ya Samagoal ni hatari, ameendelea kuwaacha mbali wapinzani wake kwenye mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora Ligi Kuu nchini humo.

Mabao mawili aliyounga Ochoa, yamemfanya kufikisha jumla ya mabao, 19 kwenye kilele cha uongozi wa ufungaji Ubelgiji, wanaomfuata ni Hamdi Harbaoui wa Waregem mwenye mabao 14 na Landry Dimata ambaye anaichezea Anderlecht kwa mkopo Wolfsburg mwenye mabao 13.

Mabao hayo yamemfanya awe nyuma ya Lionel Messi wa Barcelona mwenye mabao 21 katika La Liga nchini Hispania.