Al Ahly yatua alfajiri Dar tayari kuivaa Simba

Muktasari:

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Alexandria, Simba ilichapwa mabao 5-0 na Al Ahly

Dar es Salaam.Timu ya Al Ahly imewasili saa 10 alfajiri leo Jijini Dar es Salaam ikiwa na wachezaji 21, tayari kwa mchezo wa marudiano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba, Jumanne saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

Timu hiyo iliondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Cairo mnamo saa 4 usiku kwa saa za Misri sawa na Saa 5 usiku kwa saa za Tanzania.

Msafara huo ulitumia saa 5 angani na kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam mnamo saa 10 alfajiri.

Katika msafara huo kocha wa Al Ahly, Martin Lasarte amesafiri na kikosi cha wachezaji 21, akiwemo beki Yasser Ibrahim aliyekuwa majeruhi katika mchezo uliopita.

Al Ahly kwa sasa inaongoza kundi ikiwa na pointi saba, tatu zaidi ya AS Vita Club, na nne mbele ya Simba inayoshika nafasi ya tatu, huku JS Souara ikiwa ya mwisho na pointi zake mbili.

Habari njema kwao ni kurejea kwa majeruhi beki Yasser Ibrahim aliyekosa mechi tatu zilizopita, pamoja na Mohamed Sherif naye amesafiri na kikosi hicho.

Katika upande mwingine nahodha Hossam Ashour ataikosa mechi hiyo pamoja na Walid Azaro, Ahmed Fathi, Walid Soliman, na Marwan Mohsen kutokana na kuwa majeruhi.

Kikosi:

Makipa: Sherif Ekramy, Mohamed El Shennawy, and Ali Lotfi.

Mabeki: Saad Samir, Rami Rabia, Ayman Ashraf, Ali Maaloul, Mahmoud Wahid, Mohamed Hany, Yasser Ibrahim.

Viungo: Amr El-Sulya, Karim Nedved, Hamdi Fathi, Islam Mohareb, Hussein El-Shahat, Ramadan Sobhi, Nasser Maher, Mohamed Sherif, Hesham Mohamed.

Washambuliaji: Salah Mohsen, Junior Ajayi.