Siri nzito yagubika mkutano wa MO Dewji leo

Muktasari:

Huo utakuwa ni mkutano wa kwanza kwa MO Dewji kuzungumza na waandishi wa habari tangu Simba ilipobadili mfumo wa uendeshaji wake mwaka jana.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Mfanyabiashara Mohammed Dewji leo anatarajia kufanya mkutano na waandishi wa habari mnamo saa 8 mchana jijini Dar es Salaam.

Huo utakuwa ni mkutano wa kwanza kwa MO Dewji kuzungumza na waandishi wa habari tangu Simba ilipobadili mfumo wa uendeshaji wake mwaka jana.

Hadi wakati huu ambao zimebaki saa chache kabla ya kuanza kwa mkutano huo, bado Dewji hajaweka wazi nini ambacho atakizungumza ingawa ni wazi kwamba kitahusu klabu ya Simba.

Hisia za wengi ni kuwa huenda mkutano wa Dewji ukajikita zaidi katika ushiriki wa Simba kwenye mashindano mbalimbali hasa yale ya Afrika tangu ilipoanza kuwa chini ya mfumo wa kampuni lakini pia utekelezaji wa mipango ya muda mfupi ambayo aliiainisha wakati alipotangazwa rasmi kuwa mwekezaji ndani ya klabu hiyo.

Chini ya mfumo wa kampuni, Simba imefanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo inashika nafasi ya tatu kwenye kundi D nyuma ya Al Ahly na AS Vita Club huku JS Saoura ikishika mkia.