Mayay awakosha mashabiki Simba

Muktasari:

Ni mchezo wa 15 kwa Simba ambayo imecheza idadi ndogo zaidi ya mechi kwenye Ligi Kuu kutokana na viporo vyake vinavyotokana na ushiriki wake katika mashindano ya kimataifa

Dar es Salaam. Mchambuzi wa soka na nyota wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa 'Taifa Stars', Ally Mayay amegeuka kivutio kwa mashabiki wa Simba baada ya kumpatia mmoja wapo maji ya kunywa muda mfupi wakati wa mapumziko.

Chupa hiyo ya maji ilikuwa imeanguka chini jirani na benchi walilokaa Simba na Mayay ambaye alikuwa eneo ambalo hukaa wafanyakazi wa Azam Media ambao hushughulikia masuala ya urushaji wa mechi, aliiokota chupa hiyo na kumpa shabiki huyo ambaye alikuwa anamuita na kumuomba amletee.

Baada ya kufanya kitendo hicho, mashabiki hao wa Simba walianza kushangilia huku wakilitaja jina lake, wakati huo yeye mwenyewe akielekea eneo ambalo alikuwa amekaa.