Dakika 45: Simba yaichakaza Mwadui mabao 3-0

Muktasari:

Simba imeitangulia Mwadui katika kipindi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwa kuifunga mabao matatu ndani ya dakika tisa.

Dar es Salaam. Mtego wa kuotea umeiponza Mwadui imejikuta ikifungwa bao la mapema kwa kichwa na mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na kuwafanya mabingwa watetezi kwenda mapumziko wakiwa mbele 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

Licha ya kuanza vibaya kwa viungo wao kupoteana ndani ya dakika 20 za kipindi cha kwanza, Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 21 ya mchezo baada ya Haruna Niyonzima kupiga krosi iliyomaliziwa na Kagere.

Wakati krosi hiyo ikichongwa, mabeki wa Mwadui,  walionekana kumpisha Kagere wakidhani ameotea kabla ya kustuka na kukuta amemalizia mpira huo kwa wepesi.

Dakika tano baadae Simba walijipatia bao lingine kupitia kwa Mzamiru Yassin huku la tatu likifungwa dakika ya 29 na John Bocco.

Bao la kwanza ndilo lililoonekana kuwaondoa Mwadui ambao waliuanza vizuri mchezo wa kuwanyima uhuru viungo wa Simba kumiliki mpira kwenye eneo hilo.

Kikosi cha Simba leo kinamabadiliko makubwa ukilinganisha na kile kichocheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, jijini Cairo nchini Misri.

Katika eneo la kiungo, wameanza Haruna Niyonzima,  Mzamiru Yassin ambao hawakuanza kwenye mchezo uliopita ambapo wanasaidiana na James Kotei na Clotus Chama.

Safu ya ushambuliaji ya Simba inanaongozwa na nahodha wao, John Bocco ambaye hakuanza mchezo uliopita na Meddie Kagere.

Upande wa mabeki ni Zana Coulibaly, Mohammed Hussein 'Tshabalala' Paul Bukaba ambao hawakuanza mchezo uliopita ambao wanacheza na Pascal Wawa huku kipa akiwa Aishi Manula.