Lukaku: Man U? Raha sana Mourinho kaondoka

MANCHESTER, ENGLAND. Mshambuliaji Romelu Lukaku amesema kwamba maisha ya Manchester United kwa sasa ni raha sana tangu Jose Mourinho alipofukuzwa kazi.
Straika huyo alisema kwamba chini ya kocha wa muda Ole Gunnar Solskjaer kila mchezaji amekuwa mwenye furaha na jambo hilo limewafanya kuwa na moyo wa kuitumikia timu yao na wanafanya hivyo bila ya kuchoka. Lukaku alisema wachezaji sasa kila mmoja anafurahia kuichezea Man United hata Paul Pogba muda wote amekuwa akitasabamu.
"Tangu aondoke Jose Mourinho, mambo ni tofauti, kumekuwa na mtazamo chanya zaidi na watu wamekuwa na furaha kubwa, wakitasababu kila wakati. Hilo linasaidia sana," alisema Lukaku.
"Pogba? Kwa sasa anafuraha. Mazoezini amekuwa akiambiwa kila wakati kwamba, anapofurahi basi hata timu inashinda. Baada ya hapo wote tunacheka na kiwango cha kila mchezaji kimekuwa juu.
"Paul, Marcus, mimi mwenyewe, Anthony, kila mtu yupo tayari kwa kupambana na kila mchezaji anajaribu kumwonyesha kocha kwamba yupo tayari wakati wote.
"Tunavyofanya huko mazoezini inatufanya kila mchezaji aamini kwamba yeye ndiye atakayecheza, kwa sababu ubora wa kila mtu upo juu. Lakini, zaidi ya yote kitu kinachosimama mbele ni timu."