Ole Gunnar ashuhudia PSG ikinyukwa na Lyon

Muktasari:

  • PSG itakuwa na kibarua kizito mbele ya Man United Feb 14, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa

Paris, Ufaransa. Kocha Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer alikuwa jukwaani akishudia Paris Saint Germain ikipokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Lyon.

Kocha huyo wa miamba ya Old Trafford alitumia muda huo kuangalia PSG kabla ya Man United kuwavaa miamba hiyo ya Ufaransa katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa.

Solskjaer alikuwa jukwaani akiwa amevalia kofia ya rangi ya kijivu na koti jeusi la mvua kutokana na hali ya hewa ya Ufaransa kwa sasa.

Katika mchezo huo Paris St-Germain ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Angel Di Maria, ambaye shuti lake lilimpita Anthony Lopes na kujaa wavuni dakika saba.

Moussa Dembele alifunga bao la kusawazisha kwa Lyon baada ya kipa wa PSG, Alphonse Areola kushindwa kuokoa krosi iliyopigwa na Leo Dubois.

Matokeo yalikuwa 2-1 wakati Nabil Fekir alipofunga bao la pili kwa penalti baada ya beki Thiago Silva kumchezea vibaya mshambuliaji Dembele.

Pamoja na kipigo hicho, PSG bado inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 10 mbele ya Lille huku wakiwa na mechi mbili mkononi.

Lyon wenyewe wamejikita katika nafasi ya tatu baada ya kupata pointi hizo tatu.