Kakamega yamtimua kocha, Wanga apewa mikoba

Tuesday January 29 2019

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

Mombasa. Mashabiki wa soka wa Mkoa wa Pwani na hasa wa Kaunti ya Mombasa leo walishtushwa walipopata habari ya Kocha Mkuu wa Kakamega Homeboys FC, Paul Nkata kutemwa kwa madai ya kujihusisha na kupanga matokeo ya mechi.

Klabu hiyo imetangaza kuwa straika wao mkongwe, Allan Wanga na goalikipa David Juma wataisimamia timu kwa muda.

Kulingana na Mwenyekiti wa Kakamega Homeboys FC Cleophas Shimanyula, uchunguzi unafanywa pia kwa wachezaji saba wanaodaiwa walihusika na kuihujumu timu hiyo.

“Wanga na Juma watasaidiana na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu yetu, Eliud Omukuyia wakati tunapoendelea kufanya uchunguzi kwa wanasoka saba wanaodaiwa wanahusika kuifanyia hujuma timu,” alisema Shimanyula.

“Tumeshapiga ripoti polisi na kurikodi ushahidi na pia tumeandikia Shirikisho la Soka la kenya (FKF) kuhusiana na jambo hilo,” alisema Shimanyula ambaye alidai Nkata alimtumia mwanasoka George Mandela kuwasihi wenzake sita kuuza mechi kwa kati ya Sh50,000 na Sh200,000 kwa kila mechi.

Shimanyula alidai baadhi ya mechi anazodai Nkata alipanga matokeo yake ya kushindwa ni zile zilizochezwa Januari 2 na 19 dhidi ya Sony Sugar na Mathare United mtawalia. Kwenye mechi hizo, Homeboys ilishindwa 2-1 na Sony Sugar uwanja wa Awendo na ikatandikwa 3-2 na Mathare United uwanja wa Kasarani.

Nkata aliwahi kuwa kocha wa Bandari FC katika msimu wa 2017 ambapo timu hiyo haikufanya vizuri na alitimuliwa msimu uliopita ambapo Ken Odhimabo alishikilia madaraka kwa muda kabla ya kuajiriwa kwa Bernard Mwalala katikati ya msimu wa 2018.

Advertisement