Kariobangi bingwa, mashabiki Yanga, Simba wagawana timu

Sunday January 27 2019

 

By Oliver Albert

Dar es Salaam. Kariobangi Sharks imetwaa ubingwa wa SportPesa baada ya kuifunga Bandari FC kwa bao 1-0, huku mashabiki wa Simba na Yanga wakigawana timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kariobangi Sharks imejinyakulia kitita cha dola 30,000 ( sawa Sh69 milioni za Tanzania), mshindi wa pili Bandari imepata dola 20,000 (Sh46 milioni), wa tatu Simba imelamba dola 7500 ( Sh17.2 milioni) na mshindi  wa nne Mbao imeambulia dola 5000( Sh11.5 milioni).

Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kuvutia bao la Kariobangi Sharks likifungwa dakika ya 61 na Mwenda Harrison.

Harrison alifunga bao hilo baada ya kuwachama mabeki wa Bandari FC na kuachia shuti lililomshinda kipa Faruk Shikalo.

Licha ya Bandari kumiliki mpira na kushambulia mara kwa mara kipindi cha kwanza, lakini safu ya ulinzi ya Kariobangi ilikuwa imara.

Kipindi Cha pili Kariobangi Sharks walirejea mchezoni kwa nguvu na kufanya mashambulizi mengi golini kwa wapinzani wao na kufanikiwa kupata bao hilo la ushindi.

Kivutio katika mchezo huo ni baada ya mashabiki wa Simba kuishangilia Kariobangi Sharks na wale wa Yanga kuipa sapoti Bandari FC inayonolewa na mchezaji wao wa zamani Bernard Mwalala.

Mashabiki wa Simba waliishangilia Kariobangi Sharks kwa sababu Bandari iliwafunga katika mchezo wa nusu fainali kwa mabao 2-0.

Mashabiki wa Yanga waliishangilia Bandari kwa sababu Kariobangi Sharks iliwafunga katika robo fainali kwa mabao 3-2.

Advertisement