Yanga yaichapa Mwadui, yaiacha Simba kwa pointi 20

Muktasari:

Yanga ni timu pekee ambayo haijafungwa katika Ligi Kuu Bara hadi sasa msimu huu.

Dar es Salaam. Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutokufungwa baada ya kuichakaza Mwadui kwa mabao 3-1 usiku huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuiacha Simba kwa tofauti ya pointi 20.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Ibrahim Ajib, Amis Tambwe na Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku bao l kufutia machozi kwa Mwadui likifungwa na Salum Aiyee.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 53 baada ya kucheza mechi 19, na kuwaacha mabingwa watetezi Simba kwa tofauti ya pointi 20 baada ya kucheza mechi 14, wakati Azam ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 kabla ya mchezo wake wa kesho dhidi ya Ruvu Shooting.

Tofauti ya pointi 20 kati ya Yanga na Simba itawalazimi mabingwa hao watetezi wenye viporo saba kushinda mechi zote huku ikiomba watani zao wapoteze ili kuwafikia.

Katika mchezo huo timu zote zilianza kwa kasi huku wote wakionekana kutaka bao la mapema katika mchezo huo.

Dakika 3, Salim Aiyee alipiga shuti ndani ya boksi baada ya kuonganishiwa pasi na Ditram Nchimbi, hata hivyo shuti hilo lilipanguliwa na Klaus Kindoki na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Ndani ya dakika 11, Yanga hawakuliona lango la Mwadui mpaka dakika hiyo hiyo Ajib alifunga bao la kuongoza kwa faulo baada ya Mrisho Ngassa kudondosha nje kidogo ya eneo la 18.

Hata hivyo Mwadui waliendeleza mashambulizi na dakika 14 Ditram Nchimbi alipiga shuti, lakini lilitoka pembezoni kidogo kwenye goli lao.

Safu ya ulinzi kwa upande wa Yanga ilikuwa ikikatika mara kwa mara kiasi ambacho waliwaruhusu washambuliaji wa Mwadui, Ditram Nchimbi na Salim Aiyee kuingia ndani ya 18 mara kwa mara.

Yanga ilipata penalti dakika 17 baada ya beki wa Mwadui, Frank John kufanya madhambi kwa Tambwe, lakini hata hivyo penalti hiyo iliyopigwa na Ajib iliishia mikononi mwa Arnold Massawe.

Kipa wa Yanga, Klaus Kindoki katika mchezo huu alikuwa na makosa ya mara kwa mara kiasi ambacho kilimlazimu kocha Mwinyi Zahera kufanya nae kikao kifupi wakati mchezo huo ukiendelea.

Mwadui walizidi kuutawala mchezo kwa kufanya mashambulizi ya haraka haraka kiasi ambacho kilionekana kuwapa presha safu ya ulinzi Yanga, lakini hata hivyo hawakuweza kuweka mpira wowote wavuni.

Mshambuliaji wa Yanga, Ajib alitolewa nje na mwamuzi Fikiri Yusuph baada ya kuvaa tait rangi tofauti lakini alipobadilisha alirejea uwanjani.

Yanga licha ya kuongoza kwa goli moja walikuwa wanacheza kwa kujilinda zaidi huku wakishambulia kwa kuvizia wakati Mwadui walikuwa wakifunguka na kushambulia kwa mfululizo.

Yanga ilipata bao la pili baada ya Tambwe kuunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Ajib na kuwanyanyua mashabiki kwa bao hilo.

Baada ya bao hilo kuingia wachezaji wa Mwadui walikaa kikao cha takribani sekunde 20 kujadiliana kilichotokea uwanjani hapo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kushambulia zaidi na dakika 50 walikosa goli baada ya kipa wa Mwadui, Arnold Massawe kupiga pasi fupi na Tambwe aliwahi mpira huo hata hivyo alishindwa kuuweka wavuni.

Yanga walibadilisha mbinu katika dakika 45 za kipindi cha pili kwani walikuwa wakifunguka na kushambulia tofauti na walivyokuwa wanacheza katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Feisal Salum aliwainua mashabiki wa Yanga baada ya kuachia kombola kali dakika 57 na kutinga moja kwa wavuni akipokea pasi kutoka kwa Ibrahim Ajib.

Beki Gadiel Michael alionyeshewa kadi ya njano dakika 61 baada ya kumfanyia faulo beki wa Mwadui Revocatus Richard.

Yanga ilifanya mabadiliko dakika 65 kwa kumtoa Haruna Moshi 'Boban' na kuingia Andrew Vicent 'Dante' kwenda kuimarisha safu yao ya ulinzi ambayo ilikuwa ikiwaruhusu washambuliaji wa Mwadui kusogea, wakati huo huo Mwadui walifanya mabadiliko kwa kumtoa Jean Girukwishaka na kuingia Wallace Kiango.

 

Mwadui walikosa goli la wazi baada ya kiungo Otu Joseph kupiga pasi ya mwisho kwa Salim Aiyee ambaye alikutana nao ndani ya boksi na kumtoka kipa Klaus Kindoki lakini hata hivyo alipiga shuti lilioenda nje.

Dakika 71 beki Paul Godfrey akinyiwa faulo na beki Emmanuel Simon na kuonyeshewa kadi ya njano, hata hivyo upande wa wachezaji hawa walikuwa wamekamiana tangu kipindi cha kwanza.

Dakika 76 Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuntoa Paul Godfrey ambaye alionekana kuumia na kulala chini na kuingia Juma Abdul.

Mwadui walipata goli dakika 82 baada ya Ditram Nchimbi kupiga krosi ndani ya boksi na kumaliziwa vizuri kwa kichwa na Salum Aiyee, wakati huo huo Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Mrisho Ngassa na kuingia Said Makapu.

Baada ya mchezo kumalizika kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alikana kutofurahishwa na matokeo ya mchezo huo, huku akionekana kuwa na hasira zaidi baada ya kocha wa makipa Yanga, Juma Pondamali kumsogelea na kuanza kuzozana naye.