Ulimwengu kivutio, Saoura ikitua

Muktasari:

Hii ni mara ya pili kwa Thomas Ulimwengu kuja nchini akiwa na timu ya nje ya nchi baada ya kufanya hivyo mwaka 2016 akiwa na TP Mazembe

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania anayechezea JS Saoura ya Algeria, Thomas Ulimwengu amekuwa gumzo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati timu hiyo ilipotua usiku huu.

Ulimwengu ambaye amejiunga na timu hiyo hivi karibuni alijikuta akizongwa na kundi la waandishi wa habari na watu wengine waliokuwepo uwanjani hapo.

Baada ya kutoka nje ya geti la abiria wanaowasili Ulimwengu ambaye alianza kufuatwa na kundi hilo alielekea katika duka la kubadilishia fedha lililopo uwanjani hapo na kukaa kwa muda kabla ya kutoka na kuzungumza na wanahabari kisha akaelekea kwenye basi la Taifa Stars ambalo ndilo liliwabeba kuwapeleka hotelini.

Akizungumzia mchezo huo wa Jumamosi, Ulimwengu alisema timu bora itapata matokeo uwanjani.

"Sisi tumejiandaa kwa ajili ya mchezo huo na wao Simba kama wako vizuri tutaona uwanjani. Kikubwa nafurahi kucheza nyumbani," alisema Ulimwengu.