Waarabu wa Simba watua na mbwembwe Uwanja wa Ndege

Muktasari:

Hii ni mara ya kwanza kwa Saoura kuja Tanzania tangu ilipoanzishwa mwaka 2008

Msafara wa timu ya JS Saoura ya Algeria umeingia na mbwembwe za aina yake leo usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo imekuja na utitiri wa watu zaidi ya 60 ambao miongoni mwao walikuwemo wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi, viongozi wa timu, waandishi wa habari sambamba na mashabiki wachache wa timu hiyo.

Timu hiyo ambayo iliwasili Uwanjani hapo mnamo saa 4 usiku na ndege binafsi ya kukodi, ilianza kutoka kwenye geti la abiria wanaowasili kuanzia saa 4.30 usiku baada ya kumaliza taratibu za uhamiaji wakiwa na rundo la mizigo ambayo ililazimika kubebwa na gari maalum lililoandaliwa.

Mizigo hiyo ilijumuisha maji ya kunywa, vifaa vya mazoezi, madawa pamoja na sare ambazo watazitumia.