Mrithi wa Mourinho kitendawili kipya Manchester United

Muktasari:

Mourinho akiwa na Man United amefanikiwa amefanikiwa kutwaa mataji mawili Kombe la Ligi na Europa Ligi katika miaka miwili na nusu aliyokaa Old Trafford

London, England. Baada ya siku 895, hatimaye kocha Jose Mourinho amefungasha virango vyake Manchester United, maswali vichwani mwa mashabiki wa klabu hiyo inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ni nani atakayeirithi mikoba ya Mreno huyo.

Manchester United imemtimua Mourinho baada ya kipigo cha mabao 3-1 toka kwa Liverpool Jumapili, Hii imedhihirisha fununu zilizokuwepo kuwa mechi hiyo ndiyo iliyokuwa kipimo cha hatima ya kibarua chake.

Kocha huyo Mreno ameiacha klabu ikiwa na pointi 19, amekuwa miongoni mwa makocha walioshindwa kuirejesha Man United katika hadhi yake tangu alipostaafu kocha nguli Alex Ferguson, licha ya wadau wa soka kuwa na imani naye.

Miongoni mwa makocha wanaopigiwa chapuo la kurithi mikoba ya Jose Mourinho ni Mauricio Pochettino wa Tottenham kwa sasa amekuwa akitajwa mara kwa mara tangu wakati wa  kocha Louis van Gaal ambapo mashabiki waliamini Pochettino ndiye angeshika usukani kuliongoza jahazi.

Kikwazo kikubwa ni kwamba Pochettino amesaini mkataba wa miaka mitano Mei mwaka huu kuendelea kukinoa kikosi cha Tottenham.

Zinedine Zidane alishangaza ulimwengu alipoamua kujiuzulu kuifundisha Real Madrid baada ya kuiongoza kuchukua ubingwa wa klabu bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mfululizo Mei mwaka huu.

Mfaransa huyu anatazamwa kwa macho ya karibu na wadau wa soka hasa ikizingatiwa mpaka sasa hana klabu yoyote anayoifundisha.

Kocha mwingine anayeangaziwa jicho la karibu na wadau wa soka ni Antonio Conte. Kocha huyu anasemekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuifundisha Manchester United.

Conte ana historia nzuri ya mataji ambapo ana mataji manne ya ligi akiwa na miaka 49 tu, kocha huyu wa zamani wa Juventus na timu ya taifa ya Italia anaweza kuwa na moto kama wa Mourinho jambo ambalo bodi ya timu itapaswa kumuongoza sawasawa.

Wengine ni Laurent Blanc aliyeifundisha Paris Saint-German kwa mafanikio makubwa sana na baadaye kupumzika kwa miaka miwili sasa, Leonardo Jardim aliyefukuzwa katika klabu ya Monaco kwa kutofanya vizuri. Wachambuzi wa mambo wanasema hiyo haiwezi kuwa kikwazo kwake kukabidhiwa United.

Pia, wamo Michael Carrick aliyekipiga Manchester United tangu mwaka 2006 ingawa anasemekana kutokuwa na uzoefu wa kutosha.

Wengine ni Ryan Giggs aliyekuwa kocha wa muda United mwaka 2014 na Arsene Wenger kocha mkongwe aliyeondoka Arsenal kwa mafanikio makubwa.

Pamoja na wadau kutabiri majina mengi ya makocha wanaodhani watapewa nafasi ya kukinoa kikosi cha Manchester United ni Zinedine Zidane na Mauricio Pochettino ambao kura nyingi za wadau wa soka zinawaangukia.