Makambo atupia usiku Yanga yaichapa Ruvu Shooting

Muktasari:

Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutokufungwa katika Ligi Kuu msimu huu baada ya kuichakaza Ruvu Shooting kwa mabao 3-2.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Heritier Makambo alifunga bao dakika 94, na kuiongoza Yanga kuichapa Ruvu Shooting kwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali mshambuliaji Makambo aliyepokwa bao la mapema na Amissi Tambwe alifunga bao lake la 9 akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahimu Ajib.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 44, wakifuatiwa na Azam (40) na Simba ikiwa na pointi 27.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Tambwe dakika 11, baada ya Makambo kumchambua kipa kabla ya Mrundi huyo kuwahi mpira na kumalizia wavuni, lakini Fullzulu Maganga aliisawazishia Ruvu Shooting katika dakika 31 na kufanya timu hizo kwenda mapumziki zikiwa sare 1-1.

Katika mchezo huu Shooting ilikimiliki mpira na kuanzisha mashambulizi kuliko Yanga lakini hata hivyo dakika za lala salama walionekana kupoteana na kuanza kuruhusu Yanga wakicheza karibu na lango lao.

Dakika 48, Shooting ilikosa bao la wazi baada Haji Mwinyi kupiga kichwa na mpira kuambaambaa hata hivyo Maganga alikosa umakini katika kumalizia.

Katika safu ya ulinzi kwa Yanga ilizidi kukatika baada ya kutoka Andrew Vicent, kwani maelewano ya Abdallah Shaibu 'Ninja' na Cleofas Sospeter ilionekana kutotulia.

Yanga ilifanya mabadiliko dakika 57 kwa kumtoa Papy Tshishimbi na nafasi yake ilichukuliwa na Pius Buswita  wakati Haji Mwinyi nafasi yake ikichukuliwa na Deus Kaseke, nao Shooting walimtoa Baraka Mtuwi na kuingia Mussa Said.

Mabadiliko ya Yanga yalimfanya Jafari Mohammed aliyekuwa anacheza kama kiungo kurudi kucheza katika beki ya kushoto alipotoka Haji Mwinyi, huku Kaseke aliyeingia kuchukua nafasi ya Haji Mwinyi akienda kucheza nafasi ya Jafari.

Dakika 63 Yanga ilikosa bao baada ya Feisal Salum kumpigia pasi Makambo ambapo mabeki wa Shooting waliona kama ameotea, hata hivyo shuti la Makambo liliishia mikononi mwa kipa Abdallah Rashid.

Kiungo Feisal Salum alipewa kadi ya njano dakika 65  baada ya kumfanyia madhambi William Patrick, wakati huo huo Shooting walifanya mabadiliko kwa kumtoa Maganga na kumuingiza Alinanuswe Martin.

Kiungo Pius Buswita alipewa kadi ya njano dakika 71 baada ya kumfanyia madhambi Mussa Said.

Yanga walionekana kutaka kupata goli la kuongoza kwani walifosi mashambulizi kwa spidi lakini mipangilio yao ilikuwa ikishindwa kukamilika.

Dakika 76 Ibrahim Ajib aliumiliki mpira kwa takribani sekunde 5 kisha aliuchpou mpira na kupita juu ya mabeki wa Shooting na kukutana na Makambo, hata hivyo Makambo alishindwa kuuweka mpira huo wavuni.

Kipa wa Shooting, Abdallah Rashid alionekana kuigiza kuumia na mwamuzi Fikirini Yusuph alimpa kadi ya njano dakika 78 na mpira ulipootusha ilitokea pasi za gonga ni kugonge kwa Yanga na kiungo Feisal Salum alipiga shuti kali na kutinga wavuni na kuifanya Yanga kuwa mbele kwa 2-1.

 

Shooting nao licha kwamba walikuwa nyuma kwa 2-1 walizidi kusongesha mashambulizi na dakika 83, Said Dilunga alifanyiwa madhambi na Sospete nje ya  18 na mpira ulikuwa faulo ambayo ilipigwa na Amis Tambwe aliunawa mpira ndank ya 18 na kuwa penalti iliyopigwa na Said Dilunga na kutinga wavuni na kufanya matokeo kuwa 2-2.

Dakika 90 Shooting ilifanya mabadiliko kwa kumuingiza Hamis Kasanga na kumtoa William Patrick, wakati huo huo Yanga ilipata faulo baada ya Paul Godfrey kufanyiwa madhambi nje ya 18, lakini faulo hiyo ilipigwa na Ajib na Makambo alionganisha mpira huo kwa kichwa na kuingia wavuni na kufanya mchezo kumalizika 3-2.