Cheki waliotoka na kuingia dirisha dogo la usajili Bongo

Muktasari:

Dirisha dogo la usajili likiwa limefungwa jana usiku, klabu mbalimbali zimejiimariasha kwa kuongeza wachezaji katika maeneo ambayo yalionekana kuwa na mapungufu ya haraka

Dar es Salaam.Usiku wa kuamkia leo Jumapili, dirisha dogo la usajili lilifungwa huku klabu zikiwa bize kukimbizana na muda kabla ya kufungwa rasmi.

Licha ya mazingira magumu ya kiuchumi kwa klabu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kutowepo kwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo, kuna maboresho ya vikosi  ambayo yamefanyika yakiongozwa na vigogo, Simba, Yanga na Azam.

Wapo ambao walikuwa wakisajili kimya kimya na wengine wakivuta mashine zao mpya kwa vishindo kutokana na nguvu kubwa ya fedha walizonazo kipindi hiki.

Mwanaspoti inakuletea wachezaji ambao wamehama kutoka klabu moja na kwenda nyingine. Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa kwa timu zote 20, zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

AFRICAN  LYON

Upande wa African Lyon wameondokewa na nyota wao Haruna Moshi aliyejiunga na Yanga, Adam Omary ambaye ameshasaini Prison licha ya kwamba Zamunda bado anazuia barua ya kumuachia (Releasing Letter).

Wakati huo huo klabu hii imemchukua kwa mkopo Swaleh Abdallah (Azam) na Adil Nassor (Coastal Union) ili kuongeza nguvu katika mzunguko wa pili.

AZAM  FC

Kikosi cha Azam FC  kimetumia dirisha dogo la usajili kwa kumnasa Obrey Chirwa aliyevunja mkataba wake kwenye klabu  ya  Nogoom El Mostakbal ya Misri aliyotua akitokea Yanga.

Kundi kubwa la wachezaji wa Azam, wametoka kwa mikopo akiwemo, Mbaraka Yusuf aliyejiunga na Namungo ya daraja la kwanza, Wazir Junior (Biashara Utd), Ditram Nchimbi (Mwadui Fc).

BIASHARA  UNITED

Kikosi hiki kinachoburuza mkia kimekuwa kikitengeneza nafasi nyingi lakini katika upande wa umaliziaji kumekuwa na tatizo kubwa ambalo wamkuwa wakihangaika nalo.

Katika kuhakikisha kwamba tatizo hilo linaisha, wameamua kumchukua kwa mkopo Wazir Junior kwani wanaamini anaweza kuleta nguvu kwenye safu ya ushambuliaji akisaidiana na Lambele Jerome.

COASTAL  UNION

Kikosi hiki amabcho anakichezea msanii ali Kiba, hakijafanya usajili wa maana zaidi ya kumuongeza Miraj Adam peke yake kwenye nafasi ya ulinzi.

Lakini pia imemtoa kwa mkopo kiungo mshambuliaji wao, Adil Nassor ambaye amejiunga na African Lyon baada ya kukosa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi hiko cha Tanga.

JKT  TANZANIA

Wajeda jeda hawa wameendeleza undugu na wenzao, Ruvu Shooting baada ya kumtoa kwa mkopo mshambuliaji wao Idd Mbaga.

Hii ni mara ya pili kwani JKT Tanzania ilimpeleka kwa mkopo Shooting beki wao, Renatus Morris huku straika wa Shooting, Abdulrahman Mussa akiingia JKT Tanzania kwa mkopo.

KMC

Timu  ya  Manispaa ya Kinondoni ( KMC), yenyewe imewanasa, Mohammed Rashid kutoka Simba kwa mkopo, Elias Maguli aliyekuwa huru, Salum Chuku aliyevunja mkataba wake Singida United.

LIPULI

Matola hajataka kukuitanua sana kikosi chake kwani usajili alioufanya ni kumuongeza kiungo mnyanmbulifu Babu Ally ambaye amevunja mkataba na kikosi chake cha Mbeya City.

KAGERA SUGAR

Kassim Khamis  mkataba wake na Prison umemalizika amejiunga na Kagera Sugar kwaajili ya kuitumikia.

MBAO  FC

Kocha Amri Said yeye ameamua kufanya marekebisho kuanzia kwenye benchi lake la ufundi kwa kuanza kumchukua Ally Bushiri ili aweze kusaidiana nae katika benchi hilo.

Katika upande wa wachezaji wamemsajili Jackson Gervas (African Lyon), Erick Murilo kwa mkataba wa miaka miwili (Stand Utd), Abdul Haji na Metacha Mnata wakijiunga kwa mkopo kutoka  (Azam).

MBEYA CITY

Klabu hii imeondokewa na nyota wake Haruna Shamte na Babu Ally ambao mikataba yao imevunjika baada ya kukubaliana kwa pande zote mbili, huku Babu Ally akijiunga na Lipuli Fc.

Wakati huohuo kiungo wao mwingine Daniel Joram yeye ameenda kujiunga na Namungo Fc inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza.

MWADUI FC

Kocha Ally Bizimungu ameziba pengo la Charles Ilamfya ambaye amejiondoa katika kikosi hiko kutokana na madaia yake yaliyopo kwenye mkataba.

Bizimungu aliamua kumsajili kwa mkopo Ditram Nchimbi ili kuongeza nguvu katika nafasi hiyo ambayo ameona itapwaya baada ya Ilamfya kuondoka.

NDANDA FC

Yusuph Mhilu aliyejiunga na Ndanda ya Mtwara kwa mkopo wa miezi sita ni miongoni mwa mastaa  waliotua kwenye klabu hiyo kipindi hiki cha usajili, mchezaji mwingine aliyejiunga nakikosi  Augustino Samson kutoka African Lyon na kocha Khalid Adam aliyeenda kurithi mikoba ya Malale Hamsini aliyetimkia Alliance.

RUVU SHOOTING

Jina kubwa lililotua Ruvu Shooting ya Pwani ni Emmanuel Martin ambaye ametokea Yanga ambako makataba wake unatajwa kuwa ulimazika na hakuwa kwenye mipango ya  kocha wa  mabingwa hao wa Kihistoria, Mwinyi Zahera.

Pia imemchukua kwa mkopo mshambuliaji Idd Mbaga kutoka kwa mapacha wao JKT Tanzania.

SIMBA  SC

Wekundu wa Msimbazi, Simba wao wamemsajili mchezaji mmoja tu kipindi cha  usajili ambaye ni Zana Coulibaly alitua kwenye klabu hiyo kwa ajili ya kuziba pengo la Shomari Kapombe mwenye majeraha.

SINGIDA UNITED

Walima alizeti, Singida United, wananyota kadhaa wapya wa kigeni ambao imewasajili. Nyota hao ni Gilbert Mwale kutoka, Gift Chikwangala na Jonathan Daka wote ni raia wa Zambia.

Waliondoka Singida ni Salum Chuku, Eliuter Mpepo ametimkia Zambia huku awali kabla ya dirisha kufunguliwa wakina Peter Manyika JR na Jamal Mwambeleko wakitimkia zao Kenya kwenye klabu ya KCB.

STAND UNITED

Klabu hii imeondokewa na mshambuliaji wao Brigimana Blaise aliyejiunga na Mwadui, Erick Murilo aliyejiunga na Mbao, lakini nao hawakuwa nyuma kwani waliingia sokoni na kumchukua mshambuliaji Sixtus Sabilo ambaye alikuwa akiichezea Majimaji.

TANZANIA PRISONS

Baada ya mambo kwenda kombo ndani ya kikosi hiki wameamua kuimarisha kikosi chao kwa kufanya usajili wa winga Adam Omary kutoka katika kikosi cha African Lyon.

Wakati huo huo kipa Metacha Mnata ambaye alikuwa akiichezea timu hiyo kwa mkopo aliamua kuondoka na kurejea kwa mkopo katika kikosi cha Mbao Fc ambacho alikuwa akikitumikia kabla hajenda Prison tena kwa mkopo.

YANGA SC

Usajili wao mkubwa ambao wameufanya ni kumsajili kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye alikuwa akiitumikia klabu ya African Lyon.

Hata hivyo imeondokewa na winga wao Emmanuel Martin aliyejiunga na Ruvu Shooting baada ya mkataba wake kumalizika huku ikimtoa kwa mkopo mshambuliaji wao kinda Yusuf Mhilu kwenda Ndanda.