Wema Sepetu alikoroga tena Instagram

Muktasari:

Wakati huohuo ikiwa ni takribani miezi miwili tangu aingie katika sakata hilo, majuzi amerejea mitandaoni kwa kuweka taarifa za biashara zake na filamu aliyoshiriki ya Saa Mbovu itakayoonyeshwa hivi karibuni katika king’amuzi cha Azam.

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mitandaoni ya kijamii, inayomkabili msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu, bado haujakamilika na sasa itasikilizwa tena Januari 28, mwakani.

Wakati huohuo ikiwa ni takribani miezi miwili tangu aingie katika sakata hilo, majuzi amerejea mitandaoni kwa kuweka taarifa za biashara zake na filamu aliyoshiriki ya Saa Mbovu itakayoonyeshwa hivi karibuni katika king’amuzi cha Azam.

Wema ambaye ni Miss Tanzania wa mwaka 2006, anakabiliwa na shtaka moja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili Kaima aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Hivyo akaiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi wa shauri utakuwa umekamilika ama la.

Baada ya wakili huyo kueleza hayo, Wakili wa Wema, Ruben Simwanza alidai kuwa hana pingamizi.

Msanii huyo alipofikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu, Novemba Mosi, 2018, kujibu shtaka hilo.

Hata hivyo baada ya kusomewa shtaka hilo na kukana shtaka, alitakiwa kutoweka video zinazohusiana na ngono wala maneno yoyote yenye muelekeo huo katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.

Tangu aachiwe kwa dhamani amekuwa akiweka matangazo pekee katika ukurasa wake wa Instagram mpaka mwanzoni mwa wiki hii alipoweka matangazo ya duka lake la mavazi ya watoto na filamu.

Tangazo la filamu lilionekana kuwavutia watu kwani liliambatana na lilioonyesha filamu aliyocheza mwanamitindo Hamisa Mobetto.

Katika kesi hiyo Wema anadaiwa kuwa Oktoba 15, mwaka huu katika maeneo mbali mbali ya jiji la Dar es Salaam alichapisha video ya ngono na kusambaza katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.