Kakolanya anatoka, Shikalo anaingia Yanga moto uleule

Muktasari:

Kakolanya amejiondoa katika kikosi cha Yanga tangu aliporejea nchini akitokea Lesotho alipokuwa kwa mchezo wa timu ya taifa

Dar es Salaam. Mabosi wa Yanga hawataki mchezo, mara baada ya kuona kipa wao namba moja Benno Kakolanya anazingua kwa kutaka kuvunja mkataba kutokana na kudaki stahiki zake wamepiga hesabu za maana na wakaamua kuleta kipa mwingine.

Yanga ambao mpaka sasa katika mechi 15 wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara tisa huku wakitumia makipa watatu Nkinzi Kindoki aliyefungwa manne katika mechi nne, Ramadhani Kabwili amefungwa matatu na Kakolanya akiruhusu mawili tu.

Katika kuhakikisha mambo yanakwenda sawa haswa katika lango lao kuwa na kipa imara mabosi hao wa Yanga wametua nchini Kenya kufanya mazungumzo na kipa Farouk Shikalo ambaye anikipiga Bandari ya Ligi Kuu nchini humo.

Habari kutoka katika kamati ya usajili ya Yanga iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Hussein Nyika wameshamaliza mazungumzo na Shikalo ambaye ni kipa namba mbili wa timu ya Taifa ya Kenya.

Mmoja wa kigogo wa Yanga alisema wameshamaliza mazungumzo na kipa huyo na kinacho subiriwa ni kumpelekea mkataba na kusaini kabla ya dirisha dogo kufungwa Desemba 15.

"Tumeshamaliza kila kitu na Shikalo anachosubiri ni mkataba tu kutoka kwetu na tutaamua asaini hapa au tumfate kule kule kwao Kenya na kabla ya usajili kufungwa tutashusha vifaa vingine viwili vya maana," alisema mtoa taarifa huyo ambaye aliomba jina lake lisiwekwe wazi.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema alishangazwa kupata taarifa za kipa wake Kakolanya kuwa meneja wake ni Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi Simba jambo ambalo katika soka na upinzani wa timu hizo mbili lilivyo siyo zuri.

"Kwangu siwezi kuacha kufanya mambo mengine ya msingi nikaanza kumtafuta au kumpigia simu Kakolanya aweze kurudi katika timu kisa madai yake wakati wachezaji kibao karibia wote wanadai," alisema.

"Kama kocha ndio nitakuwa na maamuzi ya mwisho katika nafasi yake kama nitaleta kipa mwingine au kuwatumia waliokuwepo," alisema Zahera.