Kipa msomi Ligi Kuu afunga ndoa Mwanza

Muktasari:

Kuna wakati mlinda mlango wa zamani wa Toto Africa na Mbao FC zote za Mwanza aliingia kwenye mtego wa Klabu za Simba na Yanga kumtaka lakini aligoma kwa madai kuwa ana majukumu na shule.

Dar es Salaam. Mlinda mlango wa zamani wa Toto Africa na Mbao FC za Mwanza, Erick Ngwengwe amefunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu Pascaria.

Ngwengwe mlinda mlango msomi mwenye Shahada ya Udhamiri ya Histori chuo cha Sauti na sasa anamalizia Shahada ya udhamiri ya Mipango na Usimamizi atakayopata Desemba 14, Chuo Cha Mipango.

Mlinda mlango huyo anayekumbukwa na tukio kubwa moja Mbao FC ilipocheza na Simba wakafungwa mabao 3-2. Mchezo huo Mbao alikuwa anaongoza mabao 2-0 mpaka dakika ya 82, lakini Simba walitumia dakika nane kusawazisha na kufunga la ushindi.

Tukio hilo lilizua wasiwasi na kipa huyo kuundiwa kamati ya kuchunguzwa na yeye akaamua kujiweka pembeni akamilishe mambo yake ya soka, lakini kabla aling'ara kutokana na ubora wake akiwa na Toto Africa na hata Mbao FC kabla ya mchezo huo.

Jumamosi iliyopita aliamua kuhalalisha na mchumba wake huyo na kufanya sherehe kubwa katika Ukumbi wa Rock City Mall.

Amesema, anajisikia mwenye furaha baada ya kumwoa mwanamke anayempenda kwa miaka mingi na katika kipindi sahihi.

"Ndiyo hivyo mambo yamekamilika sasa ni baba wa familia. Nimefurahi kwa sababu nimebarikiwa katika kipindi sahihi nilichokihitaji,"alisema Ngwengwe.

Kwa kipindi chote cha uchezaji, Ngwengwe amekuwa kicheza mpira huku akisoma isipokuwa msimu huu tu alipoamua kukaa pembeni baada ya majukumu ya shule kuzidi.

Amesema, baada ya kumaliza anatarajia kurudi uwanjani kwa mara nyingine kwenye mzunguko wa pili wa ligi au mwakani.