KMC yakoma, Azam yashindwa kuing’oa Yanga kileleni

Muktasari:

Kutokana na matokeo hayo, Azam FC iliyocheza mechi 16, inaendelea kukaa kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 40, Yanga ndiyo vinara wa Ligi Kuu Bara wakiongoza na pointi 41, baada ya kucheza mechi 15.  Simba inayoshiriki mashindano ya kimataifa ni ya tatu ina pointi 27, baada ya kucheza michezo 12, wakati Mtibwa Sugar ambayo pia inacheza mechi hizo ni ya nne, ina pointi 23 na michezo 14.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Mzambia Donaldo Ngoma alipachika bao la kusawazisha dakika ya 85, matajiri wa Azam FC leo Jumatatu wangelala mbele ya KMC katika mchezo wao uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Ngoma alisawazisha bao hilo kwa Azam FC ambalo lilikuwa la pili na kufanya matokeo kuwa 2-2, na kuifanya timu hiyo ikiendeleza historia yake ya kutofungwa tangu msimu wa Ligi Kuu Bara uanze na huo ukiwa mchezo wa 16.

Matajiri hao ambao kwa kawaida wakiwa jijini Dar es Salaam huwa wanacheza mechi zao usiku katika uwanja wao wa Chamazi lakini huu ulikuwa tofauti kama wapo mkoani baada ya kucheza saa 10:00 jioni.

KMC wao ndiyo walikuwa wa kwanza kupachika bao kupitia kwa George Sangija katika dakika ya 18 na Azam FC wakawa watu wa kusawazisha tu. Bao hilo liligombolewa na Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyuakipachika sekunde chache kabla timu hazijakwenda kwenye mapumziko.

Kipindi cha pili kilipoanza, Rayman Mgungila akaifungia tena KMC katika dakika ya 63, kabla ya Ngoma kusawazisha katika dakika hiyo ya 85 kwa shuti la mbali akiunganisha krosi ya Enock Atta.

KMC ambayo kwa matokeo hayo yameendelea kuwabakisha nafasi ya 11 na pointi 18, baada ya Lipuli FC kuifunga Ruvu Shooting mabao 2-1, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Samora mkoani Iringa, ilicheza bila nahodha wao, Juma Kaseja ambaye yupo nchini Misri na kikosi cha timu ya taifa ya soka la ufukweni, ilionyesha kiwango kizuri na kuwapa ushindani Azam FC inayonolewa na Kocha Hans Pluijm.