Mwadui FC yanasa nyota wawili kutoka Ghana, Uganda

Muktasari:

Mwadui FC tayari imesajili wachezaji watatu kati ya watano iliyopanga kuwasajili katika dirisha dogo la usajili litakalofungwa Desemba 15

 

Mwanza. Mwadui FC imefanikiwa kunasa saini ya nyota wawili Evans Sekazza (Uganda) na Soa Benjamini kutoka Ghana kila mmoja amesaini kandarasi ya mwaka mmoja ukiwa ni usajili wa pili baada ya kumleta mshambulia Ditram Nchimbi kwa mkopo kutoka Azam FC

Kocha Mkuu wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema kutokana na mahitaji yao wameamua kuwashusha nchini nyota wawili kutoka Ghana na Uganda ili kujenga vema kikosi chake.

Bizimungu aliwataja nyota hao ni kiungo mshambuliaji Sekazza (Uganda) na mshambuliaji Soa Benjamin (Ghana) kila mmoja amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo.

“Ni mapendekezo yetu Benchi la Ufundi kuhitaji timu ifanye vizuri, tunachotaka ni kuona Mwadui inashinda kila mchezo na kwa mabao mengi, tunaamini ujio wa nyota hawa watafanya kitu," alisema Bizimungu.

Kocha huyo aliogeza kuwa baada ya kukamilisha dili hilo la nyota wa kimataifa, kwa sasa wanaumiza kichwa kumalizana na wachezaji wengine wawili ili kukiweka kikosi fiti tayari kwa kuanza kazi.

Alisisitiza kuwa kwa mwenendo walionao hivi sasa haoni timu itakayopenya miguuni mwao bila kuonja kipigo kutokana na maandalizi wanayoendelea kuyafanya na kuwaomba mashabiki kuendelea kusapoti timu hiyo.

“Mpango ni kusajili wachezaji watano, kwahiyo baada ya kumalizana na hawa sasa tunageukia wengine wawili waliobaki ambao mazungumzo yanendelea hatua za mwishoni,” alitamba Mnyarwanda huyo.