African Lyon yaikamia Mbao FC

Muktasari:

Ni mchezo wa Ligi Kuu unaotarajiwa kupigwa kesho Jumanne kwenye uwanja wa CCM Kirumba ambapo African Lyon imewatambia Mbao FC kuwa lazima washinde mchezo huo

Mwanza. Kocha Msaidizi wa African Lyon, Adam Kipatacho amesema wamekuja Mwanza kwa lengo moja la kupata ushindi dhidi ya Mbao FC kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba,Mwanza.

African Lyon kwa sasa ina pointi 11, ikiwa nafasi ya 19 kwenye msimamo wa Ligi.

Kocha Kipatacho alisema hakuna kingine wanachokitaka katika mpambano huo zaidi ya pointi tatu ambazo angalau zitawatoa mkiani.

Alisema kwa sasa hawana mwenendo mzuri hivyo timu yake imeanza kampeni kabambe ya kujinasua kutoka katika eneo la hatari kwenye msimamo wa ligi hiyo hivyo moja ya mechi ambayo ni lazima washinde ni dhidi ya Mbao FC.

“Tumeanza kampeni sasa kila mechi tunataka kupata matokeo mazuri ambayo yatafanya tutoke mkiani kwenye msimamo wa Ligi na tunaanza na Mbao FC kuhakikisha tunapata pointi tatu,” alisema Kipatacho.

Kocha huyo alisema wanajua kuwa wapinzani wao wametoka kuchezea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC na mchezo huo utakuwa mgumu kwao lakini watapambana ili kuweza kuondoka na ushindi.

“Huu mpambano utakuwa mgumu kwani wapinzani wetu wanataka kulipiza kisasi kwani walifungwa mchezo uliopita, lakini sisi tumejiandaa vya kutosha tunataka alama tatu,” alisema Kocha huyo.