He! Mo Salah kakataa tuzo huko England

Muktasari:

  • Mo Salah aliikataa tuzo hiyo na kuamua kumpa mchezaji mwenzake, Mwingereza James Milner. Mwandishi wa Sky Sports, Greg Whelan alimfanyia mahojiano Salah ya ushindi wake wa tuzo hiyo kisha kugoma kuichukua na badala yake akampa Milner.

LIVERPOOL, ENGLAND.MOHAMED Salah juzi Jumamosi alipiga hat-trick wakati Liverpool ilipojipigia Bournemouth mabao 4-0 na kukamatia usukani wa Ligi Kuu England.

Baada ya mechi hiyo, fowadi huyo wa kimataifa wa Misri, Mo Salah alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi na alipopewa tuzo yake, akawashangaza wengi baada ya kuikataa.

Mo Salah aliikataa tuzo hiyo na kuamua kumpa mchezaji mwenzake, Mwingereza James Milner. Mwandishi wa Sky Sports, Greg Whelan alimfanyia mahojiano Salah ya ushindi wake wa tuzo hiyo kisha kugoma kuichukua na badala yake akampa Milner.

Mo Salah alisema: “Hapana. Mechi 500. Napaswa kumpongeza sana Milner kwa namna alivyodumu kwenye soka lake.

“Anastahili hii tuzo kwa siku ya leo na amekuwa kwenye kiwango kizuri. Nina imani tutashinda kitu tukiwa pamoja msimu huu, hivyo siwezi kuichukua hii tuzo.”

Milner alicheza mechi yake ya 500 kwenye Ligi Kuu England na katika mchezo huo wa juzi alitumika kwenye nafasi ya beki wa kulia. Milner ni kiraka, anamudu namba kibao uwanjani.