VIDEO: Rweyemamu ashinda mashindano ya gofu ya MCL-LBGC

Saturday December 8 2018

 

By Majuto Omary

Dar es Salaam.Mchezaji wa gofu maarufu, Mohamed Rweyemamu ameshinda mashindano ya ligi ya klabu ya Lugalo yajulikanayo kwa jina la Lugalo Breakfast Golf Community (LBGC) yaliyomalizika ijumaa kwenye uwanja wa gofu wa klabu ya TPDF, Lugalo.

Rweyemamu alishinda kwa mikwaju 76 dhidi ya mpinzani wake nyota, Foti Gwebe aliyemaliza kwa mikwaju 91. Mshindi wa tatu katika mashindano hayo ni Joseph Tango  kwa kupiga mikwaju 79 na kumshinda mpinzani wake, Balozi Sai Kaphale aliyemaliza kwa mikwaju 86.

 Rweyemamu ulikuwa na siku ya furaha sana kwa ushindi huo uliokwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa mke wake na ‘ku-dedicate’ ushindi huo kwake.

“Ninafuraha sana kwa ushindi huu, kwanza kabisa ni kuadhimisha sherehe ya kuzaliwa kwa mke  wangu, pili hatua ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kudhamini mashindano haya, ni faraja kubwa sana kwangu,” alisema Rweyemamu.

Alisema kuwa haikuwa kazi ndogo kushinda kutokana na kiwango cha mpinzani wake, Gwebe ambaye alicheza vizuri pamoja na kumaliza katika nafasi ya pili. Rweyemamu alizawadiwa kikombe na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL.

Kwa upande wa wanawake, mcheza gofu maarufu  Angel Eaton alimshinda nyota mwingine wa kike, Hawa Wanyeche kwa staili ya ‘countback baada ya nyota hao kupiga mikwaju 72 kila mmoja.

Eaton alisema kuwa alipata ushindani mkubwa sana kutoka kwa Wanyeche ambaye ni mmoja wa wachezaji wa timu ya Taifa.

Kwa upande wa kundi la Lugalo younger golfers,  Francis Ekeng  alishinda kwa mikwaju 71 dhidi ya Cloudy Mtavanga aliyepata mikwaju 72 huku kwa kundi la Laki Si Pesa , John H alishinda kwa kupiga mikwaju 70 na kumshinda Balozi Kalino aliyemaliza kwa mikwaju 75.

Kwa upande wa kundi la Wazee Poa , Boniface Nyiti alimshinda Joseph Tairo kwa kumaliza kwa mikwaji  77 dhidi ya  84 na Pricilla Karobia alishinda Maryanne Hugo kwa mikwaju 86 upande wa kundi la MMS baada ya kumchapa mpinzani wake kwa mikwaju  95.

Mkurugenzi wa MCL, Fancis Nanai alisema kuwa amefurahishwa sana na viwango vya wachezaji na watadhamini mashindano hayo kila mwaka.

 “Tumevutiwa sana na mashindano haya, kwa kweli yametupa mwamko mkubwa na hivyo tutaendelea kuyadhamini kwa lengo la kuendeleza mchezo na kutumia fursa ya kukutana na wadau wetu,” alisema Nanai.

Advertisement