Kocha Tenerife: Lugha kikwazo kwa Chilunda

Thursday December 6 2018

 

Tenerife, Hispania. Kocha wa CD Tenerife, Jose Luis Oltra amesema mshambuliaji wake Shabaan Chilunda anakumbana na kikwazo cha lugha katika maisha yake ndani ya klabu hiyo.

Kocha Oltra alisema Chilunda ni mchezaji mzuri, lakini anapata wakati mgumu kutokana na kutojua lugha hivyo anashindwa kuelewa baadhi ya maelekezo anayopewa.

“Kikwazo kikubwa kwa Chilunda ni lugha, katika kupokea maelekezo, ila uwezo wake ni mzuri.

“Tunatakiwa kuwa na subira kwake kwa sababu anakitu kikubwa, hivyo baada ya muda anaweza kuwa bora zaidi,” alisema Oltra wakati akizungumzia maandalizi yao ya mechi ya kesho dhidi ya Extremadura UD.

Nchini Hispania wanatumia lugha kihispania pamoja na kilatino katika mawasiliano jambo linalomtatiza Chilunda ambaye anajua kuzungumza Kiswahili na Kiingeleza.

Chilunda amejiunga na Tenerife mwanzoni mwa msimu huu, tangu wakati huo bado hajapata namba ya kudumu ila amekuwa akitumiwa kama mchezaji wa akiba.

Chilunda amejiunga na CD Tenerife kwa kusaini mkataba wa mkopo wa miaka miwili na mara baada ya kutambulishwa siku iliyofuata akaanza mazoezi yake ya kwanza mchana kwenye kituo cha Ciudad Deportiva Javier Perez.

Akiwa na furaha nchini humo, Chilunda alisema ametua Tenerife kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye msimu mpya wa Segunda na alienda mbali kwa kusema mbali na kufunga atashirikiana vyema na wachezaji wenzake kwa kutengeneza nafasi za mabao.

Nilikuwa mwenye furaha kubwa tangu niliposikia CD Tenerife wananitaka nijiunge nao. Nitacheza kwa nguvu na kwa kiwango kizuri, hilo siyo tatizo kwangu, japokuwa najua Hispania itakuwa tofauti, ila nitazoea kwa haraka.

Advertisement