Tamasha la Fiesta linakuja Dar kabla ya kufunga mwaka

Muktasari:

Kauli ya Kusaga kuhusu ujio huo hilo limekuja siku 11 baada ya kutangaza kuwa tamasha la Tigo Fiesta halitafanyika.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga amesema kuwa tamasha la Fiesta litafanyika kabla ya kuisha mwaka huu.

Kauli ya Kusaga kuhusu ujio huo hilo limekuja siku 11 baada ya kutangaza kuwa tamasha la Tigo Fiesta halitafanyika.

Hatua hiyo ilitokana na taarifa ya Manispaa ya Kinondoni iliyoeleza kupokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa walio karibu na eneo hilo kubughudhiwa.

“Wakati mwingine matatizo huibua fursa kubwa na bora zaidi, tamasha lijalo litakuwa kubwa kuliko lile la awali, wale ambao alikuja kutoka mikoani kwa ajili ya kuhudhuria shoo hiyo tutaangalia namna ya kuwapunguzia machungu kwenye tamasha hilo, ”alisema Kusaga alipokuwa akizungumzia kuhusu miaka 19 ya uwapo wa Clouds Media.

Alifafanua kuwa kutokana na tatizo lililojitokeza ambalo lilikuwa nje ya uwezo wao amefanya mazungumzo na Rais, Mkuu wa Mkoa na Mwakyembe ambao anajua wanatizama na kusikiliza Clouds waangalie namna bora ya kulifanya.

Alisema siyo tamasha hilo kuna matamasha mengi yanakuja, “Kuna tamasha la Wasafi Festival, Summer Jam nasikia inarudi, muziki mnene, kutakuwa na matamasha hadi 10 kwa mwaka ambayo ni bilioni za fedha zinatengenezwa hapo inapaswa kuwe na namna ya kuyaendesha.

“Sisi tupo tayari kwa kushirikiana na wadau tulio nao kujenga uwanja wa ndani utakaochukua watu 10,000 na kuendelea kwa ajili ya haya matamasha , mikutano ya dini, kwaya na vitu kama hivyo, ”alisema Kusaga.

Alisema haya yote yanahitaji ushirikiano wa Serikali na kupata sehemu ya kufanya hivyo.

“Ukisema leo nikafanye tamasha Tanganyika Packers ambako hakuna miundombinu ya kutosha si kweli na itakuwa ngumu, kwa sababu miundombinu bado tutahangaika, ”alisema.

Alisema tamasha hilo wanalipeleka kimataifa ambapo nchi nyingi zimelikubali kama ambavyo limefanyika nchini Rwanda.

Alisema wamefanya mazungumzo na nchi za Umoja wa Falme ya Kiarabu (UAE) ambako kote amelikubali.

Akizungumza kuhusu Clouds Media itakuwa wapi ndani ya miaka 10 ijayo amesema “10 ni midogo Clouds hata baada ya miaka 20 ijayo itakuwa namba moja na yeye kama mkurugenzi na mwanzilishi wake hatokubali ishuke kuwa namba mbili, ”alisisitiza.

Kuhusu kuibuka kwa redio za burudani na ujio wa matamasha alisema wao ndiyo walifungua njia na wanajipongeza kwa hilo, lakini pia ni changamoto kwao ya kuhakikisha wanafanya kilicho bora zaidi kila siku.