Mbao FC yanoa makali Mtwara kuikabili Azam

Muktasari:

Wakati klabu ya Mbao FC ikijiandaa kuchuana na Azam FC klabu hiyo imeanza kujiweka imara kwa kucheza na timu za mikoani.

Mtwara. Mbao FC imeichakaza Kiromba FC kwa mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika halmashauri ya mji Nanyamba, Mtwara ikiwa ni maandalizi yao kuelekea mchezo wake dhidi ya Azam FC utakaochezwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Chamanzi Complex Jijini Dar Es Salaam.

Kocha mkuu wa Mbao FC, Amri Said amesema wameanza kwa kucheza na timu za mikoani kwa ajili ya mazoezi na kujipima sambamba na kuibua vipaji vipya.

“Michezo hii ni muhimu kwa sababu inawapa wachezaji wangu maarifa na mbinu zaidi za kufunga, lakini tumeweza kuona vipaji vikubwa,” alisema Said

Mbunge wa jimbo la Nanyamba, Abdullah Chikota amesema mchezo huo umesaidia wananchi wa jimbo lake kuimarisha mshikamano na kujiweka fiti.

“Kwanza umejenga hamasa kwa vijana watu kucheza kwa bidii ili waweze kujiunga na timu kubwa, lakini inawaimarisha kwa sababu umeona wamejijengea kujiamini kumbe na wao wanaweza,”alisema Chikota

Baadhi ya mashabiki wa Kiromba FC wamesema mchezo huo utasaidia wachezaji wao kuonyesha vipaji vyao sehemu mbalimbali.

“Sisi hatushiriki ligi yoyote, lakini leo tumeweza kuandika historia ya kipekee kwa sababu timu yetu wala haiko katika daraja la tatu, tumejifunza mengi,”alisema Ramadhan Abdul