Singida, Arusha zang’ara Morogoro Marathon

Muktasari:

Mbio hizo ziliwashirikisha wanaridha 670, ambako washindi kwanza kwa wanaume alipata Sh400,000 na wanawake alipata Sh100,000

Morogoro. Wanariadha wa mikoa ya Singida na Arusha umeng’ara katika mbio za Morogoro Marathon 2018 kilometa 21, huku wanaridha wenyeji Morogoro wakiambulia kuingia nafasi ya 10 bora mkoani hapa.

Mshindi wa kwanza katika mbio za kilometa 21 wanaume ni Marco Joseph kutoka Singida aliyetumia saa1:05:50 nafasi ya pili ikachukuliwa na Faraja Razaro wa jeshi Arusha kwa kumaliza saa 1:06:04.

Wakati upande wa wanawake mshindi wa kwanza katika mbio hizo za kilometa 21 ni Amina Mohamed alitumia saa1:21:47 na nafasi ya pili alikuwa Lozalia Fabian aliyemaliza kwa saa 1:23:59 huku wote wakitokea Arusha JKT.

Mjumbe wa kamati ya Ufundi shirikisho la riadha Tanzania, Tullo Chambo alisema mbio za Morogoro Marathon 2018 zimeonyesha mwanga kwa kuibua wanariadha wengine wapya na kuanza kuonekana.

Chambo alisema mchezo wa riadha umekuwa na mvuto na katika kalenda ya shirikisho la riadha Tanzania kuna matukio ya mbio za barabarani zinazohusisha kilometa 21 na 42.

“Mbio za barabarani mbio fupi na ndefu ndio mbio za mwisho kwa mwaka huu kwa mbio za Morogoro Marathon na Kigamboni na tunawapongeza waandaji na wadau mbalimbali hiyo kwetu sisi ni faraja.”alisema Chambo.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi zao, Marco Joseph na Amina Mohamed walisema wameshiki mbio hizo bila kufahamu zawadi za mshindi wa kwanza.

 

Joseph alisema kuwa mashindano yajayo ya Morogoro Marathon 2019 waandaaji wanapaswa kutangaza zawadi za mshindi wa kwanza kama sehemu ya kivutio kwa wanariadha.

“Kuna baadhi ya zawadi nimekuja kuziona leo kama hivi ving’amuzi na mashindano yajayo ya mwaka 2019 waandaaji watangaze mapema zawadi za washindi na hii itakuwa kivutio kwa wanariadha wengi,”alisema Joseph.

Naye Amina alisema kuwa wanawake, wasichana wajitokeze kushiriki mashindano mbalimbali licha ya kuimarisha afya, lakini michezo ni ajira.

Amina alisema kuwa yeye amekuwa akifaidika na michezo ikiwemo riadha kwa kumpatia kipato kinachosaidia kukidhi maisha.

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza mbio za kilometa 21 wanaume amepata zawadi ya sh400,00 na king’amuzi cha dstv wakati mshindi wa pili akipata sh250,000  na mshindi wa tatu, Mathayo Jeremiah akiondoka na sh150,000.

Wanawake mbio za kilometa 21, mshindi wa kwanza alizawadiwa sh100,000, mshindi wa pili sh50,000 ambapo mbio hizo ziliwashirikisha wanaridha 670 kwa mbio za kilometa tano na 21.

Mbio hizo zilianza kutimua vumbi uwanja wa Jamhuri saa 12 asubuhi na kuhitimishwa uwanja huo saa nne asubuhi.