Huko Yanga mambo ndo yanaanza upya

Muktasari:

Yanga inatakiwa kufanya uchaguzi wake mkuu Januari 13, jambo lililozua mvutano baina ya TFF na klabu hiyo juu ya hatma ya mwenyekiti Yusuf Manji

Dar es Salaam.VIONGOZI wa matawi wa Yanga wamezidi kukomaa na kutokubali uchaguzi wao kusimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakisema hawatakubali kuvunja katiba yao lakini kamati yao ya utendaji ikafanya maamuzi mawili katika kufanyia kazi maelekezo ya serikali.

Akizungumza katika kutangaza uamuzi huo Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Siza Lyimo alisema wameamua kuyafanyia kazi maagizo ya serikali kwa kuijazia watu kamati yao ya uchaguzi.

Lyimo alisema katika kazi hiyo kamati yaoa ya utendaji imewaogeza mawakili watatu kuwa sehemu ya kamati hiyo na tayari wameshaiwasilisha TFF na baraza la michezo.

Akitaja walioongezwa kuwa ni Makili Edward Mwakingwe, Godfrey Mapunda na Samuel Mangesho ambao wataungana na kamati iliyopo ikiongozwa na mwanasheria mkongwe Samuel Mapande akisaidiwa na Jabir Katundu, Daniel Mlelwa na Mustapha Nagal.

"Tumeamua kuwaongeza hao ili kusudi sasa kamati yetu iwe na nguvu ya kuweza kusimamia uchaguzi wetu kama ambavyo katiba yetu inaelekeza,"alisema Lyimo akiwatangazia viongozi wa matawi ya Yanga na baraza la wadhamini la klabu hiyo jana.

Lyimo aliongeza kuwa katika kikao chao cha jana pia walifanyia kazi maelekezo ya serikali kumchagua kiongozi wao katika wajumbe wa kamati ya utendaji waliosalia wakati huu sintofahamu ya kurejea kwa mwenyekiti wao Yusuf Manji ikifanyiwa kazi.

"Tumeamua hilo kulifanyia kazi kwa kumchagua Samuel Lukumay kuwa kiongozi wetu katika wajumbe saba tuliosalia na kaimu wake nitakuwa mimi, Siza Lyimo.

"Katika kuchaguana huku mwenzetu Thobias Lingalangala hakushiriki baada ya kuwa mzito kuja kujadiliana katika vikao lakini tunasikia anapita katika maofisi ya watu akipeleka mambo yanayohusu klabu yetu.

"Nasema wajumbe wako saba kutokana na wenzetu wanawasahau wajumbe wenzetu watatu wa kuteuliwa ambao ni Majid Seleman, Mack Antony na Mohamed Nyenge.

Aidha katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya klabu hiyo wajumbe wa kamati ya matawi walionyesha kusikitishwa na hatua ya serikali kupitia vyombo vya usalama kusitisha mkutano mku wao wa dharura uliokuwa ufanyike jana.

Mwenyekiti wa matawi kanda ya Kinondoni Shabani Omar alisema Yanga haiko tayari kuvunja katiba yao kwa kukubali uchaguzi kufanyika chini ya TFF.

Omari alisema mkutano wao uliokuwa ufanyike jana ulikuwa na umuhimu na umuhimu mkubwa kwa kuupa dhamana mkutano mkuu kutengua maamuzi yao yaliyopita.

"Hatukuwa na njama ya vurugu lakini tunasikitika ambao wamekwenda kuiongopea dola,mkutano wetu ulikuwa wa amani ndiyo maana uongozi wetu ukaomba vibali vyote na tulitaka kusikia uamuzi wa mkutano mkuu,"alisema Omar.

Naye Mjumbe wa baraza la wadhamini jaji mstaafu John Mkwawa alisema Wanayanga wanapaswa kuendeleza utulivu na kwamba wanasubiri ruhusa ya serikali kuendelea na mkutano wao.

"Yanga haijawahi kugombana na serikali wala mamlaka zote za juu tumekuwa watiifu na tutaendelea kuwa watiifu lakini tulitaka kujadiliana mustakabali wa klabu yetu kwa utulivu,niwaombe wanachama watulie tunayafanyia kazi,"alisema Mkwawa.