Mbonde bado kidogo tu Simba

Muktasari:

Tangu msimu huu wa 2018/19 uanze beki wa Simba, Salim Mbonde hajajiunga na programu na wenzake kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mguu wa kulia.

Dar es Salaam. Mashabiki wa Simba wajiandae tu kumuona nyota wake, Salim Mbonde akirejea tena uwanjani kukinukisha.

Si mnajua Mbonde tangu asajiliwe Msimbazi akitokea Mtibwa Sugar misimu miwili iliyopita amecheza mechi chache ikiwamo moja ya msimu uliopita kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Mechi ya mwisho ya Mbonde aliyocheza Simba ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar, wakati wakikabidhiwa ndoo ya ubingwa msimu uliopita na Rais John Magufuli kabla ya kutoka akiwa hajatumia hata dakika 10 tena akilia kutokana na kujiumiza tena.

Baadaye Simba, walimpeleka Mbonde kwenda kutibiwa Afrika Kusini, lakini tangu msimu huu uanze hajaonekana hata katika mazoezi ya pamoja na wenzake.

Daktari wa Simba, Yasin Gembe alisema Mbonde anaendelea vizuri, japo kwa sasa hawezi kucheza kutokana na kutokuwa fiti.

"Mbonde anaendelea vizuri, lakini bado hajawa fiti kucheza mechi hivi karibuni kadri siku zinavyoendelea atarejea kwenye majukumu yake kama kawaida," alisema Dk Gembe.