Yanga: Kwa Bomba huyu Simba mjipange, Zahera afichua mazito

Muktasari:

Bomba ni winga anayejua kusumbua kwa mguu wake wa kushoto na kwamba akicheza winga ya kulia, kushoto haya nyuma ya mshambuliaji wa mwisho mashabiki wa Yanga watashangilia kazi yake

Dar/ Mbeya.VINARA wa Ligi Kuu, Yanga jana mchana walitua kibabe Mbeya na kulifunika jiji hilo kwa shangwe za wanachama na mashabiki kibao waliojitokeza kuipokea, huku Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera aliamua kufichua siri za winga wao mpya Ruben Bomba.

Kocha Zahera amefichua mziki wa winga huyo Simba yote inatulia kwa sababu ni mchezaji mmoja matata ambaye awapo uwanjani na ukakosea kumzuia ni lazima akulize.

habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, Zahera alifanya kikao na mabosi wa Kamati ya Usajili, kisha akasimulia vitu vitamu alivyonavyo winga huyo mpyakiasi cha mabosi hao kutamani kama angeruhusiwa kucheza mechi ya kesho dhidi ya Prisons.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hussein Nyika alisema katika kikao chao Zahera amewaambia kuwa Bomba ni winga hatari na kwamba bosi huyo na wenzake watajuta kuchelewa kumpata, kwani wakiwa naye hakuna klabu itakayowazuia.

Nyika alisema Zahera amewaambia, amemleta mtu anayemjua ufanisi wake wa kazi na kwamba kuna kitu kikubwa kimeongezeka katika safu yao ya ushambuliaji baada ya Bomba kutua Jangwani.

Nyika aliongeza, Bomba ni winga anayejua kusumbua kwa mguu wake wa kushoto na kwamba akicheza winga ya kulia, kushoto haya nyuma ya mshambuliaji wa mwisho mashabiki wa Yanga watashangilia kazi yake.

Alisema kama mambo yatatulia katika utata wa uongozi wao Bomba atasaini haraka kutokana na wanataka kikosi chao kiwe na nguvu kubwa katika mzunguko wa pili.

"Tumekutana na kocha leo (jana) kabla ya kuondoka kwenda Mbeya ametuambia Bomba ni winga ambaye anakuja kuwafundisha mawinga wa hapa jinsi ya kutumia mguu wa kushoto," alisema Nyika.

"Hatuna wasiwasi na anachokisema kocha wetu amekuwa akililia kwa muda mrefu akitaka tumletee winga na sasa kampata na katika maelezo yake tulitamani angekuwa uwanjani Jumatatu kucheza dhidi ya Prisons, ila ndiyo hivyo kanuni haziruhusu."

 Kikosi chatua kibabe

Katika hatua nyingine unaambiwa kikosi cgha vinara hao wa Ligi Kuu, Yanga jana mchana kilitua kibabe jijini Mbeya na kupokewa kwa shangwe tayari kwa mchezo wao wa keshoJumatatu dhidi ya wenyeji wao maafande wa Prisons.

Baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo waliojitokeza kwa wingi waliilaki timu hiyo na kuanzisha maandamano makubwa kusindikiza kwenda hoteli watakayofikia.

Yanga ilitua saa nane hivi, huku Kocha Mwinyi Zahera alisema, mchezo wao ujao dhidi ya Prisons sio wa kubeza kutokana ukweli wapinzani wao wamejiimarisha katika safu ya ulinzi.

"Tunashukuru tumetua salama Mbeya na jukumu letu kwa sasa ni kusaka ushindi wa pointi tatu, kwani vijana wapo kamili licha ya baadhi ya wachezaji sijaongozana nao kutokana na kuwa majeraha na sababu zao binafsi," alisema Zahera.

Zahera alisema Yanga imeshindwa kuambatana na wachezaji nane wenye matatizo mbalimbali, lakini anaamini watapata matokeo Jumatatu.

"Tunashukuru kwa mapenzi waliotuonyesha mashabiki wetu wa hapa nasi tunahidi kuwafurahisha zaidi Jumatatu kwa kuwapa ushindi Uwanja wa Sokoine," alisema.