Mourinho afunguka bila pesa hakuna usajili wa maana

Muktasari:

Man United walikuwa wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na pointi zao 22 walizovuna kwenye mechi 14, ambapo walishinda sita, sare nne na vichapo vinne. Man United kwenye mechi hizo ilishinda mabao 22 na kufungwa 23

MANCHESTER, ENGLAND. AMA kweli siku zinakwenda kasi sasa. Hivi sasa Manchester United inaonekana haina uwezo tena wa kumchukua mchezaji wanayemtaka kwa sababu za ndani ya uwanja. Labda kwa pesa tu.

Kocha, Jose Mourinho amesema kwamba mambo kwenye Ligi Kuu England yamebadilika sana kiasi cha kuwafanya Man United kutokuwa na mvuto wa kusajili wachezaji wakubwa kutoka kwa wapinzani wao labda kama tu watatumia pesa nyingi.

Huko nyuma Man United ilikuwa na hadhi kubwa sana ndani ya uwanja na kipesa jambo lililokuwa likiwapa wepesi wa kumsajili mchezaji wanayemtaka na hata wachezaji wenyewe kutaka kwenda kuichezea timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.

Lakini, sasa kwenye Ligi Kuu England kumekuwa na mabilionea wengi wenye timu zao, ambao wanagawa dili za maana kwa wachezaji na hivyo kuona kama kwamba Man United si timu pekee yenye nguvu tena licha ya kuwa na utajiri mkubwa na kipato cha hali ya juu.

Mourinho ametoa mfano kwamba huko nyuma Man United iliweza kuwasajili nyota wa Tottenham Hotspur kama vile Michael Carrick na Dimitar Berbatov wakiwa kwenye viwango bora kabisa, lakini kwa sasa haina uwezo wa kumnasa Harry Kane wala Dele Alli kutoka kwenye timu hiyo.

Hivyo, Mreno huyo amedai kwamba jambo hilo linafanya wachezaji atakaowaongeza kwenye kikosi chake kuwa na viwango vya kawaida na si wale matata kama ilivyokuwa huko nyuma. Man United inapanga kufanya usajili wa nyota kadhaa kwenye dirisha lijalo la usajili wa uhamisho wa Januari.

Mourinho alisema: "Ni ngumu sana kununua wachezaji wenye viwango vya juu kwa sasa. Klabu sasa zimekuwa na nguvu sana. Timu hazitaki kuuza wachezaji wake mahiri, inaowauza ni wale wa viwango vya kawaida sana.

"Huko nyuma, klabu ndogo zilikuwa zikiteswa na zile kubwa, zilikuwa zikiiwaachia wachezaji wao bora na kuwauza, lakini kwa sasa zenyewe ndio zinanunua wachezaji bora na haziwauzi.

"Miaka michache iliyopita, mchezaji bora kabisa Tottenham alikuwa Michael Carrick. Alinaswa na Man United. Kisha akaja Berbatov. Lakini, kwa sasa nenda kwa Harry Kane, Dele Alli, (Christian) Eriksen au Son (Heung-min) kama utawapata. Huwezi kuwanasa wachezaji hao. Usajili ni mgumu labda kama tu utaamua kutumia pesa nyingi. Man United sio utamaduni wake kununua wachezaji kwenye pesa nyingi, lakini nyakati ndizo zinazolazimisha hilo kuwa."

Man United jana Jumamosi walikuwa na kibarua cha kuwakabili Southampton kwenye mchezo wa Ligi Kuu England wakijaribu kuweka mambo yao sawa baada ya kuonekana kukumbana na vikwazo vingi kwa siku za karibuni.

Presha ya kocha Mourinho imezidi kuwa kubwa kutokana na kukosa huduma ya Alexis Sanchez katika kipindi hiki muhimu kutakana na kuumia misuli Alhamisi iliyopita. Ripoti zinadai kwamba huenda akawa nje kwa kipindi kisichopungua wiki nne na kufanya kuwapo kwa pengo katika kikosi hicho licha ya kwamba amekuwa hana ubora sana tangu alipotua Old Trafford akitokea Arsenal kwenye usajili wa Januari.

Wiki iliyopita kuliwa na madai kwamba Mourinho ametibuana na mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile, lakini mwenyewe alikana jambo hilo na kusema hakuna ugomvi wowote baina yao huku kuwa na taarifa pia za kwamba supastaa huyo anapiga hesabu za kwenda kujiunga na Paris Saint-Germain baada ya kuona waajiri wake wa sasa kutokuwa na imani naye.