Redondo amfuata Boban African Lyon

Tuesday November 20 2018

 

By Oliver Albert

Dar es Salaam. Kiungo Ramadhani Chombo 'Redondo' ameungana na swahiba yake Haruna Moshi ‘Boban’ baada ya kusaini mkataba na African Lyon.

Kujiunga kwa Redondo katika klabu ya Lyon ni kuendeleza urafiki wake na Boban aliyewahi kucheza naye pamoja Simba, Mbeya City na Friends Ranges kwa nyakati tofauti.

Meneja wa African Lyon, Adam Kipatacho amesema wamemsajili Chombo wakiamini atakiongezea nguvu kikosi hicho katika michezo iliyobaki ya Ligi Kuu.

Alisema Redondo anachukua nafasi ya mshambuliaji, mfaransa,Victor Da Costa aliyetimka katika klabu hiyo mwanzoni mwa msimu pamoja na kocha Soccoia Lionel.

Da costa na kocha Lionel walitimka kutokana na madai ya ukata ndani ya klabu hiyo.

"Redondo tumesajili kutokana na kuridhishwa na kiwango chake na tunaamini atatusaidia katika ligi kuu akiungana na Haruna Moshi 'Boban',"alisema Kipatacho

Kipatacho alisema wanahitaji wachezaji wanne tu katika dirisha dogo la usajili ili kuziba nafasi mbalimbali katika kikosi chao.

Wakati huo huo timu hiyo inatarajia kuweka kambi ya wiki moja Iringa ili kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbeya City utakaofanyika Desemba 2, kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

African Lyon iko nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza michezo 13, imeshinda miwili, imetoa sare michezo mitano na kupoteza sita.

 

 

 

Advertisement