Maskini Kapombe ndiyo basi tena Simba

Muktasari:

Beki huyo ameumia kifundo cha mguu na atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu hivyo Simba watalazimika kutafuta beki wa kuziba pengo lake

Dar es Salaam. Beki wa Simba, Shomari Kapombe atakuwa nje kwa miezi mitatu baada ya kuumia kifundo cha akiwa mazoezini na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Satrs) kilichokuwa kinajiandaa mechi dhidi ya Lesotho.

Kapombe ameumia kifundo mguu wa kushoto akiwa kambini Afrika Kusini jambo lililomfanya kukosa mechi ya jana Jumapili ambayo Stars ilifungwa bao 1-0 na Lesotho.

Kutokana na majeruhi hayo Kapombe mmoja wa mchezaji tegemeo katika kikosi cha Simba chini ya kocha Patrick Aussems atakosa mechi zote mbili za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mbabane Swallow fc itakayochezwa Novemba 27 na ile ya marudiano Desemba 4.

Iwapo Simba itafanikiwa kusonga mbele Kapombe atakosa mechi mbili za raundi ya pili za Ligi ya Mabingwa zitakazochezwa Desemba 14 au 16 na marudiano Januari 11 au 13, 2019. Pia, atakosa mechi za Kombe la Mapinduzi na Kombe la Sportpesa yatakayochezwa Januari mwakani.

Katika kipindi hicho Kapombe atakosa zaidi ya mechi 10 za  Ligi Kuu zikiwamo dhidi ya Lipuli, Azam, Kagera Sugar, Coastal Union, Singida United, Prisons, Mtibwa Sugar na Mbeya City.

Kocha wa Simba Aussems alisema alipanga kusajili nyota mmoja katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, lakini kuumia kwa Kapombe lazima atafute mabadala wa nafasi hiyo ingawa hataweza kumtumia katika mashindano ya Kimataifa kwa maana usajili wa huko umeshakamilika.

“Nitafanya usajili wa beki wa kati ambaye akacheze katika nafasi ya Nyoni au kutafuta mbadala waa Kapombe ambaye atakuwa akitumika katika mashindano ya ndani, lakini kuumia kwake kutafanya timu kuwa na mabadiliko katika safu ya ulinzi,” alisema Aussems.

Msimu uliopita Simba walitwaa ubingwa Kapombe alikuwa nje nusu msimu (miezi sita) na alirudi katika mechi dhidi ya Kagera Sugar ambayo ilitoa pasi ya goli ambalo alifunga John Bocco katika ushindi wa mabao 2-0, kikosi hiko kikiwa chini ya kocha Mrundi Masoud Djuma.

Tangu Kapombe aliporudi katika kikosi cha Simba alikuwa mlinzi wa kulia katika kikosi cha kwanza kwa maana hiyo kukosekana kwake italazimika mabingwa hao kumtumia Nicholas Gyan ambaye kiasilia si mlinzi wa kulia.

Simba kama si kumtumia Gyan ambaye ameshindwa kuonesha kiwango bora akicheza katika eneo hilo huenda wakamtumia kiraka Erasto Nyoni ambaye muda mwingi Kapombe akiwepo amekuwa akicheza kama mlinzi wa kati.

Changamoto kubwa ambayo Simba watakutana nayo ni katika mashindano ya Kimataifa ambayo msimu huu watacheza Ligi ya Mabingwa Afrika jina la Kapombe limo katika orodha ya nyota wa kikosi hiko ambao watashiriki mashindano hayo huku la Gyan likiwa halimo.