Uganda yaibeba Taifa Stars safari Cameroon 2019

Muktasari:

Uganda imefuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuichapa Cape Verde

Dar es Salaam.Uganda imefanya kile kilichosubiliwa na Watanzania wengi baada ya kuichapa Cape Verde kwa bao 1-0 na kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika 2019, na kufungua njia kwa Tanzania itakayocheza mechi dhidi ya Lesotho kesho.

Uganda imefuzu kwa mara ya pili kwa fainali hizo za Afrika baada ya kuvunja mwiko 2017 nchini Gabon ikiwa ni mara yao kwanza baada ya miaka 39.

Mshambuliaji wa Patrick Henry Kaddu aliibuka shujaa wa Uganda baada ya kufunga bao pekee katika dakika 76, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Godfrey Walusimbi.

Ushindi huo unaifanya Uganda kufikisha pointi 13, ikiongoza kundi ikifuatiwa na Tanzania yenye pointi 5, Cape Verde (4) na Lesotho (2).

Kutokana na matokeo hayo Taifa Stars inaweza kufuzu fainali kabla ya mchezo wake wa mwisho iwapo itashinda kesho ugenini dhidi ya Lesotho na kufikisha pointi nane na kuivunja mwiko wa kusubiri miaka 38, kucheza fainali hizo.

Nafasi hiyo ya Tanzania inakuja baada ya CAF kubadilishwa kwa kanuni mwaka 2017, kwamba fainali za Cameroon wameongeza idadi ya timu kutoka 16 hadi 24. Kwa mfumo huo mpya kila kundi inatoa timu mbili za kwenda kushiriki mashindano hayo ya Cameroon.

Msimamo wa Kundi L

                           Pld       W    D     L      GF   GA   GD  Pts                         

1      Uganda       4        3      1      0      7      0      +6    13  

2      Tanzania              4        1      2      1      3      4      −1    5

3       Cape Verde  4      1      1      2      4      5      0      4             

4      Lesotho        4       0      2      2      2      7      −5    2

JINSI TANZANIA INAVYOWEZA KUFUZU

Tanzania inaweza kufuzu iwapo itatoa sare na Lesotho hivyo kufikisha pointi 6, na kuhitaji kushinda mechi yake ya mwisho nyumbani dhidi ya Uganda ili kufikisha pointi 9 ambazo haziwezi kufikiwa na Cape Verde wala Lesotho.

Pia, Stars inaweza kufuzu iwapo Lesotho itaifunga Tanzania, wenyeji watafikisha pointi tano sawa na Taifa Stars, na Cape Verde itakuwa ya mwisho.

Katika mchezo wa mwisho Tanzania itahitaji ushindi nyumbani dhidi ya Uganda, huku wakiomba Cape Verde iwafunge Lesotho katika mchezo utakaochezwa jijini Praia, Machi 24, 2019.

Hata hivyo, Tanzania inaweza kushindwa kufuzu iwapo atafungwa mechi hizi mbili za mwisho dhidi ya Lesotho na Uganda mbili za mwisho.

Saba zafuzu AFCON tisa zapiga chini

Timu za mataifa saba tayari zimekata tiketi ya kwenda Cameroon kucheza fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mwakani huku tisa zikiondolewa rasmi na zitajaribu tena mashindano yajayo 2021. 

Timu hizo zinaongozwa na Uganda 'The Cranes' imekuwa ya kwanza Afrika Mashariki kuingia katika fainali hizo ikitokea Kundi L, lenye timu za Tanzania, Cape  Verde na Lesotho.

Tanzania inacheza kesho Jumapili na Lesotho endapo itashinda itapita kwenda kwenda kucheza fainali hizo.

Timu nyingine zilizofuzu ni Senegar na Madagascar zikitokea Kundi A, Morocco na wenyeji Cameroon wamepita kutoka Kundi B, wakati Tunisia na Misri zimeingia baada ya  kufanya vizuri Kundi J.

Wasenegar wamepita na pointi 10, sawa na Madagascar inayokwenda kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza na kuziacha timu za Equatorial Guinea na Sudan kujaribu tena mashindano yajayo.

Morocco ndiyo vinara wa Kundi B, wamepita baada ya kufikisha pointi 10, huku Cameroon ambao ndiyo wenyeji wamesonga na pointi 8, Comoros amebaki akiwa na pointi 5, na Malawi 4.

Timu nyingine zilizofuzu ni Tunisia yenye pointi 12, sawa na Misri ambao wamewaacha  Eswatin yenye pointi 1 sawa na Niger yenye 1.

Kutokana na matokeo hayo timu za Equatorial Guinea, Sudan, Comoros, Malawi, Niger, Eswatin na Niger zimeungana na Sudan Kusini, Shelisheli na Botswana kuaga  michuano hiyo na watacheza mechi za kukamilisha ratiba tu.