Kipa Yanga afichua siri wachezaji wa Bongo kucheza chini ya kiwango

Muktasari:

Kukosekana kwa wadhamini ni moja ya sababu iliyochangia klabu nyingi za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza kuyumba kiuchumi.

Morogoro. Kipa Mufindi United ya Iringa, Benjamin Haule amesema sababu ya wachezaji wengi wanaocheza soka Tanzania hucheza chini ya kiwango kutokana na kuwa na mawazo ya namna ya kutatua majukumu ya kifamilia wawapo uwanjani.

Benjamin aliyewahi kutamba akiwa na vikosi vya Yanga SC na Moro United amesema wachezaji wengi wanategemea kipato kutoka katika soka kuendesha maisha na kutatua changamoto mbalimbali za kifamilia kwa kipato kutoka kwenye klabu.

Benjamin alisema baadhi ya ishu zinazosabisha mchezaji kucheza chini ya kiwango ni viongozi wa klabu kushindwa kutatua sehemu za changamoto za mchezaji hasa zinazohusu familia yake.

“Wachezaji wa Simba, Yanga na Azam unaweza kusema wana unafuu katika kufaidika na kipato kupitia soka, lakini wachezaji wa klabu nyingine sidhani kama vipo kwenye hali nzuri zaidi kiuchumi.”alieleza Benjamin.

Benjamin alisema kutokana na uwingi wa mashabiki wa klabu za Simba na Yanga, ndio unaotoa angalau unafaa kidogo kwa klabu mwenyeji kupata fedha za viingilio tofauti na hapo mapato yanakuwa kidogo zinapocheza klabu ndogo.

“Azam FC, Mtibwa Sugar ni klavu ambazo na zenyewe vina vyanzo vya uhakika vya mapato kwa ajili ya kuhudumia timu lakini wachezaji wake naona hawako vizuri zaidi kiuchumi kama walivyo wachezaji wa Simba na Yanga.”alisema Haule.

Akizungumza wadhamini kujitoa kudhamini klabu za ligi kuu na ligi daraja la kwanza, Haule alisema hali hiyo imekuwa ikichangia wachezaji kushindwa kuwa na kipato cha uhakika.

“Klabu ikikosa chanzo cha uhakika cha mapato kuendesha timu ndipo shida zinapoanza kutokea na kusababisha wachezaji kucheleweshewa mishahara na posho na kumfanya mchezaji kushindwa kutatua changamoto za kifamilia na mazingira hayo mchezaji hawezi kucheza kwenye kiwango kizuri,”alisema Haule.