Pep anabakia kuwa Pep, na ataendelea kuwa Pep Guardiola

Muktasari:

Bila ya kujali matumizi ya pesa lakini Pep anajua kukipata anachokitaka na kila mtu anapenda kuitazama City hata kama unataka ifungwe

MTOTO wa Marseille, Frank Lebouf, mpenda ngono kama alivyo. Aliifungia Chelsea mabao 17 akiwa kama beki wa kati. Mengine yalikuwa mazuri sana. Lakini mwishoni mwa miaka ya 1990 aliwahi kukariwa akisema ‘Mabao ya uwanjani hayajawahi kufikia mabao ya kitandani.’

Tangu lini Wafaransa walishindana starehe na Wabrazili? Ni ngumu kuamua vita hii. Wote wanapenda sana starehe. Lakini juzi juzi tu, mtoto wa Juazeiro, Bahia, Brazil, Dani Alves alikiri kwamba soka linalofundishwa na Pep Guardiola ni tamu zaidi ya ngono.

Siku mbili baada ya Alves kusema hivi, City ilipiga pasi 44 kuelekea bao la tatu lililofungwa na Ilkay Gundogan Jumapili iliyopita pale Etihad. Ilikuwa dhidi ya Manchester United sio West Brom au Wigan Athletic. Huyu ndiye Pep katika ubora wake wa hali ya juu.

Kabla ya hapo, siku chache zilizopita, Manchester City imeshutumiwa kwa kukiuka kanuni za matumizi ya pesa katika manunuzi ya wachezaji na mambo mengine. Lakini pia kuelekea katika mechi hiyo, Jose Mourinho alidai Manchester City ilikuwa imejiandaa vizuri zaidi kwa sababu ilicheza mechi mbili nyepesi dhidi ya Southampton na Shakhtar ambazo zote ilishinda kwa mabao 6-1 kisha 6-0.

Kuelekea katika mechi hiyo na hata kabla ya hapo kuna mtu amekaa sehemu anaamini  Manchester City inacheza vizuri kwa sababu imetumia pesa nyingi. Kuna anayeamini imenunua wachezaji wengi mastaa ndio maana inacheza kama inavyocheza.

Hapana. Pep ni kocha haswa. Anajua anachofanya. Kitu anachokifanya kwa sasa pale City, Ruud Gullit aliwahi kukijaribu Chelsea. Aliita Sexy Football. Vyovyote ilivyo, bila ya kujali matumizi ya pesa lakini Pep anajua kukipata anachokitaka na kila mtu anapenda kuitazama City hata kama unataka ifungwe.

Sio kila kocha unaweza kumpa Leroy Sane, Sergio Aguero, Riyad Mahrez, Silva wawili, Kevin De Bruyne, Raheem Sterling na wengineo halafu wakafanya kama wanavyofanya pale City. Hapa ndipo ambapo Pep ananikosha. Na haishangazi kwa sababu aliwahi kufanya hivyo siku za nyuma akiwa na Barca kisha Bayern Munich.

Kitu cha msingi anaamini katika falsafa yake. Anaisimamia hiyo hiyo. Nilidhani angechemsha katika Ligi Kuu ya England lakini hadithi imekuja kuwa tofauti. Amebadili vitu vichache kutoka katika kile alichokuwa anakifanya Hispania kwa ajili ya kuendana na Ligi Kuu ya England.

Bado naamini Pep ukimpa Manchester United bado itacheza kama Man City. Ukimpa Arsenal itacheza kama Man City. Ukimpa Liverpool pia bado itacheza kama Man City. Kuna ubora fulani unaweza kupungua lakini bado utamu utabakia palepale kwa sababu anaendelea kushikilia siri ya namna anachokitaka kisha anawagawia wachezaji wake halafu wanatuletea uwanjani.

Ndiyo, wachezaji wanabakia kuwa binadamu na wanatofautiana lakini Pep bado atatuonyesha aina ya kitu kilekile anachokitaka. Bado naamini ameshindwa kuchukua ubingwa wa Ulaya na Bayern Munich kisha City kwa sababu pale Barcelona licha ya ubora wa soka lake lakini kulikuwa na watu watatu wanaongeza kitu zaidi. Lionel Messi, Xavi Hernandez na Andres Iniesta.

Lakini nje ya hao, bado tunamuona Pep yuleyule katika vikosi vya Bayern na sasa Manchester City. Soka lake tamu. Anaacha alama. Wengi ambao wanaleta visingizio kwa sasa wanajinyima tu kuukubali ukweli kwamba Pep anajua kufundisha soka.

Pesa ambazo Jose Mourinho ametumia tangu afike Manchester United zilipaswa kuifanya United ipishane na City, lakini ungeweza kuona kuwa muda mwingi wa mechi walitumia kukaa katika eneo lao na kuwasubiri Manchester City. Sio suala la kwamba, Pep ametumia pesa nyingi, hapana, anajua kufundisha.

Kitu ambacho kwa sasa tunasubiri kuona ni namna ambavyo ama dunia inaweza kuiga staili hii ya soka, au inaweza kuharibu staili hii ya soka. Tunataka kuona ni lini unaweza kuwa mwisho wa staili hii ya Pep kutamba. Ameiuza bidhaa yake hii katika nchi tatu za Hispania, Ujerumani na England na inaonekana hakuna anayeweza kumzuia kiurahisi asitembe.

Pale Arsenal, Unai Emery ambaye ni shabiki mkubwa wa Pep anajaribu kuiga. Kiasi anafanikiwa na ndio maana unaona kuna wakati Arsenal inafunga mabao yenye mvuto kwa kuwa na pasi nyingi. Lakini mwisho wa siku Pep anabakia kuwa Pep.

Soka lake linatia hofu. Linatisha. Sio mtu mzuri kucheza dhidi yake. Kila siku anarudia kilekile ambacho kiliitetemesha mikono ya Sir Alex Ferguson pale Wembley usiku ule wa Mei 28, 2011. Sawa, na yeye anabakia kuwa mwanadamu wa kawaida na kuna siku anafungwa, lakini hauwezi kutamani kucheza tena na City kama kama umeifunga jana asubuhi.

Desemba mwaka jana wakati City ilipoichapa Tottenham Hotspurs mabao 4-1 katika Ligi Kuu ya England, kocha wa zamani wa Tottenham, Glenn Hoddle ambaye kwa sasa ni mchambuzi alisikika akisema “Tunaviona vitu ambavyo hatujawahi kuviona katika uwanja wa soka hapo kabla’. Ndiyo, hauwezi kubisha.