Noma! Hili la Yanga ukiliangalia ni vurugu tupu

Muktasari:

Kamati ya Yanga kabla ya kufungiwa kwa Katibu wake Bakili Makele, ilikuwa inaundwa na watu watano ambao ni Mwanasheria mkongwe Sam Mapande akisaidiwa na Daniel Mlelwa, Jabir Katundu, Mustapha Kajole.

Dar es Salaam.YANGA hakujatulia kabisa, kuna mambo hayako sawa huku malumbano kuhusiana na sakata la uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi ndani ya klabu yao.
Awali, hili halikuonekana kuwa tatizo kubwa, lakini kukosekana kwa msimamo na weledi limepelekea kuwa tatizo kubwa, ambapo kama halitachuliwa juhudi za haraka linaweza kuleta mpasua mkubwa kwa klabu hiyo kongwe.

Kiini cha tatizo
Tatizo kubwa sio ishu ya uchaguzi, ndani ya Yanga pande zote zinakubaliana na kufanyika kwa uchaguzi wa aina gani, lakini shida inakuja waliowengi hawataki kuona nafasi ya mwenyekiti inakuwa sehemu ya kugombewa wakidai mwenyekiti wao Yusuf Manji yupo.

Kwani Manji ilikuaje
Inajulikana kuwa Manji alijiuzulu kweye nafasi hiyo kwa zaidi yam waka sasa akidai afya yake imetetereka, lakini ndani ya klabu hiyo uamuzi wake haukubarikiwa na pande tatu.
Ukianza na kamati ya utendaji tena hata kabla ya kumeguka kwa baadhi kujiuzulu wote walipinga uamuzi huo wa Manji, haikutosha Baraza la Wadhamini nalo liligoma na mwisho wakamalizia mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika Juni 10, kwamba hawakubaliani na hoja hiyo ya kujiuzulu kwake.

TFF inajitundika
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia maamuzi hayo ya mkutano mkuu wa Yanga Julai 11, linatoa taarifa kwa vyombo vya habari wakimfuta kazi aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Clement Sanga kwa hoja kuwa hakuwa mtu sahihi kuongoza chombo hicho kufuatia kupoteza sifa kwa uthibitisho walioupata Yanga kuwa klabu hiyo bado inaongozwa na Manji kuwa ni mwenyekiti.
Maamuzi hayo ambayo TFF wanasema yamebarikiwa na Kamati ya Utendaji na kwamba, Sanga anavuliwa madaraka hayo kutokana na sifa kubwa aliyotakiwa kuitumia kumiliki kiti hicho ni kuwa mwenyekiti wa klabu yake na Sanga akang'oka bila ubishi.

Serikali inaingilia kati
Serikali kupitia Baraza la Michezo (BMT) likaingilia kati mgogoro wa uchaguzi huo kwa kuyakutanisha makundi matatu uongozi wa Yanga, kamati ya uchaguzi ya Yanga na kundi ambalo linaupinga uongozi wao likiongozwa na Mzee Ibrahim Akilimali.
Katika kikao hicho kilichofanyika Uwanja wa Taifa inaelezwa ndani ya kikao hicho Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe baada ya kusikiliza pande zote akaahidi kutoa msimamo ndani ya siku mbili.

BMT inachafua kabisa hali ya hewa
Baada ya kimya cha muda mrefu akaibuka Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Alex Nkenyenge akitangaza kuiagiza Yanga kufanya uchaguzi wao kwa kujaza nafasi zote hadi ya Manji huku uchaguzi huo akiutaka kusimamiwa na kamati ya uchaguzi ya TFF.
Taarifa ya Nkenyenge iliyotolewa Novemba 11 inakuwa na mapungufu ndani yake akionyesha hana taarifa sahihi katika meza yake akisema Yanga imebaki na wajumbe sita wa kamati ya utendaji, lakini pia kwa suala la Manji alipoombwa kurejea katika nafasi yake hakutoa ushirikiano.
Nkenyenge hakuwa na taarifa sahihi kwa sababu kwa hesabu zetu Yanga imebaki na wajumbe saba na sio sita ambao, katika hao wanne ni wa kuchaguliwa ambao ni Samuel Lukumay, Siza Lyimo, Thobias Lingalangala na Hussein Nyika wakati wa kuteuliwa ni Mack Antony, Majid Suleiman na Mohamed Nyenge.

Kamati ya uchaguzi
TFF na BMT wanaongeza vurugu zaidi kwa kuinyima Yanga nafasi ya kusimamia uchaguzi wao wakisema kamati yao ina mapungufu, lakini hilo linaonekana kupingwa na Yanga wenyewe
Kamati ya Yanga kabla ya juzi kufungiwa kwa Katibu wake Bakili Makele, ilikuwa inaundwa na watu watano ambao ni Mwanasheria mkongwe Sam Mapande akisaidiwa na Daniel Mlelwa, Jabir Katundu, Mustapha Kajole.
TFF na BMT ilipaswa kuja na majibu sahihi juu ya maamuzi yao juu ya mapungufu ya kamati ya uchaguzi ya Yanga kujiondolea kadhia ya uvurugaji katika hili la kamati ya uchaguzi ya Yanga kuweza kuwatosheleza wanachama wa Yanga kuliko wanavyofanya sasa hali ya kuwa katika baadhi ya vikao wanajumuika nao kama walivyokutana na Mapande pale Uwanja wa Taifa.
Pia, TFF katika kikao na uongozi wa Yanga wiki moja iliyopita wakijadiliana kuhusu uchaguzi, Kaimu Rais wake Athuman Nyamlani anachagua mwenyekiti wa muda hali ya kuwa anasahau kuwa bosi wake alishamhalalisha Manji kuwa ni kiongozi wa Yanga.
Yanga wanamlaumu Nyamlani kuwa hakuwa refa mzuri katika kesi hiyo kutokana na kuendesha vikao hivyo, wakihofu alikuwa na maamuzi yake.

Manji anarudi rasmi Yanga
Baada ya sakata hilo na ukimya wa Manji Novemba 11, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga chini ya Mwenyekiti wake Sam Mapande wanaibuka na kutangaza kurejea kwa Manji, baada ya kiongozi huyo kuandika barua rasmi akilijibu baraza hilo na wanachama kuwa ameridhia kurejea katika nafasi yake.
Ujio wa barua hiyo na ile taarifa ya TFF ya Julai 11 vinahalalisha rasmi kurejea kwa Manji kufuatia matamko hayo kuendana sawa kwa mantiki, ambapo hakuna taarifa nyingine inayokwenda kinyume na matamko.