Hasara tu: Falsafa za makocha zimewakataa

Muktasari:

Wachezaji hawa walikuwa tegemeo katika vikosi vyao kutokana na uwepo wa kocha moja na alipoondoka walipoteza namba kwa kocha mwingine

Dar es Salaam. KUNA kundi la wachezaji muhimu waliokuwa wakitegemewa kwenye baadhi ya timu huko nyuma hivi sasa hawaonekani wakicheza mara kwa mara au kutocheza kabisa.
Hali hii imewafanya baadhi ya wachezaji ambao huko nyuma walikuwa tegemeo kwenye kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' lakini hivi sasa hawamo tena.
Inawezekana ikawa ni ujio wa makocha wengine kwenye timu zao ndio uliopelekea wao kuwekwa kando au ujio wa mchezaji mwingine anayeonekana kucheza vizuri zaidi. Mwanaspoti linakuletea wachezaji ambao wameshindwa kuendena na falsafa za makocha wao.

SALMIN IDD HOZA. - AZAM
Kijana huyu alikuwa moto hasa kipindi akiwa na timu ya Mbao kwenye msimu wao wa kwanza tu tungeweza kuwaita kiboko cha vigogo licha ya kuwa tofauti na Reli ile ya Tisini kiboko cha vigogo ilipowafunga Simba na Yanga kwa goli nyingi bado Mbao nao kwa ugeni wao wakiwa Mwanza kuwafunga Yanga na Azam vigogo hawa wawili huku Simba ikiondoka na ushindi kwa tabu.
Ndani ya kikosi hicho unalikuta jina la Hoza kiungo aliyekuwa anakuja kwa kasi nafasi ya ukabaji, Hoza alifanikiwa hadi kuitwa Taifa Stars na hicho ndicho kilichowasukuma Azam kumsajili akitokea Mbao, chini ya Kocha Aristica Cioaba, Hoza alicheza michezo mingi hatua iliyompelekea mchezaji Himid Mao aliyekuwa akicheza nafasi  hiyo kuhama kwenda kulia kumpisha kijana huyo.
Kwa sasa mambo si shwari kwake ndani ya Azam chini ya Kocha Hans van der Pluijm ambaye nafasi hiyo amekuwa akimtumia Mdhathir Yahya au Frank Domayo huku falsafa ya kocha huyo ikiamini kwenye matumizi ya viungo wawili zaidi  huku akiwatumia mawinga kila kushoto na kulia , majaliwa ya Hoza ni uchezaji wake pindi siku atapoamriwa kuanza kipindi cha kwanza na yeye kucheza kwa kujituma zaidi.

ASANTE KWASI - SIMBA
Usingeweza kuwabadilisha mawazo Wanasimba, mashabiki kwa wapenzi hadi viongozi wa timu hiyo bila kuwasahau wakuu wa benchi la ufundi ukizungumzia mchezaji huyo, Kwasi alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo kuongeza kitu kwenye eneo la ulinzi.
Kwasi alikuwa zaidi ya mlinzi huku akifanikiwa kufunga magoli kadhaa hadi kuwazidi baadhi ya wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji.
Kwasi alifaa sana kwenye mfumo wa kocha aliyepita wa Simba, Pierre Lechantre na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu sana waliokuwa hapo, alicheza karibia michezo yote raundi ya pili huku akimuweka kwenye benchi aliyekuwa mchezaji bora wa ligi kuu msimu mmoja nyuma Mohamed Hussein!
Hali sasa si kama vile kwa Kwasi chini ya Patrick Aussems , benchi limemuhusu zaidi falsafa ya Aussems ni kuhakikisha timu inalinda vizuri lango huku ikishambulia kwa vipindi na hasa ndani ya mfumo wa 4-2- 1- 3 ambapo sasa zile nafasi za kumfanya afunge safari kila mara kushoto hazipo sana kwa kuwa kule juu washambuliaji wa mbele hufungua zaidi kushoto ili kupigiwa pasi nzuri za mwisho.

HADJI  MWINYI - YANGA
Mwinyi yule wa Taifa Stars vs Morocco hapa Taifa,  kumbuka lile goli la Elias Maguli krosi inatoka kushoto Wamoroco wanakufa 3-1 ,  Mwinyi yule wa Pluijm alikuwa Mwinyi kweli, usajili wake kutoka KMKM ya Zanzibar ulimaanisha Yanga walisajili mlinzi wa kushoto mwenye sifa zote, kukaba, kuanzisha mashambulizi na kutengeneza magoli ama hata kufunga.
Kimo cha Mwinyi mrefu akiutumia mguu wake wa kushoto sawa sawa vilitosha kumfanya awe chagua la kwanza kwa upande wa kushoto kwenye klabu yake na kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Taratibu Mwinyi binafsi alianza kupungua kasi yake kutokana na sababu nyingine za nje ya uwanja huku taratibu nafasi kwenye kikosi cha Taifa ikianza kuchukuliwa na Mohamed Hussein wa Simba.
Ujio wa kocha George Lwandamina ulianza kumuondoa taratibu kwenye kikosi cha kwanza na huku akitafutwa mchezaji atakayeziba vizuri nafasi yake.
Ndipo usajili wa Gadiel Michael kutoka Azam ulipokuja kuziba kabisa nafasi yake kwenye kikosi cha Yanga. Amekuja Mwinyi Zahera bado inaonekana hata kumfikiria Mwinyi kucheza hata mchezo mdogo hakuna, mfumo au falsafa ya Zahera kuona mchezaji wa sehemu ya ulinzi anapunguza au kutofanya makosa mengi kwa kukaba kwanza kwenye eneo lake ndilo linalomvuruga Mwinyi ambaye ni mzuri zaidi kwenye kushambulia kuliko kuzuia.

HARUNA NIYONZIMA - SIMBA
Mchezaji aliyekuwa ghali sana kwenye dirisha la usajili la msimu uliopita akitokea kumaliza mkataba wake Yanga na kisha kuhamia upande wa pili Simba.
Ni mchezaji mwenye kipaji maridhawa akipata mafanikio makubwa kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga alikocheza kwa takribani misimu sita, kiungo aliyekuwa chachu kubwa ya ushindi mara kadhaa wa timu ya Yanga huko nyuma akiichezea timu ya nchini kwake APR ya Rwanda. Niyonzima alicheza chini ya makocha wote waliomkuta Yanga au kuwakuta, alianza na Ernie Brants wakapita makocha wengi hapo kati hadi kipindi cha mafanikio makubwa ya kocha Pluijm misimu ya 2014 - 2016
Kuhama kwake kutoka Yanga kwenda Simba msimu uliopita hakukumuondoa kwenye kuwa mchezaji wa kutafuta namba bali kukamilisha wachezaji muhimu wa Simba, chini ya Joseph Omog hadi Pierre Lechantre hakukumtetemesha hadi pale alipopata majeraha na kumfanya kukaa nje ya kikosi kwa muda mrefu.
Msimu mpya huu umeanza na mambo mengi huku mwenyewe Niyonzima akichelewa kujiunga na kikosi kwa muda mrefu na hata aliporudi imeonekana ni wazi sasa chaguo la kuchezeshwa kwake ni kama la nne nyuma ya Clatus Chama, Hassan Dilunga na Shiza Kichuya ndani ya mfumo wa 4-2-1- 3 hali iliyompotezea namba hadi kwenye kikosi cha kwanza cha timu yake ya Taifa.

MBARAKA YUSUF - AZAM
Kwa lugha ya kimpira unaweza kusema msimu wa juzi yaani 2016/17 ulikuwa wa kwake, nyota njema ilikuwa upande wake na ilimuwakia vyema kijana huyu akiwa na Kagera Sugar chini ya kocha Mecky Mexime!
Mbaraka Yusuf alifunga kadri alivyoweza hali iliyomfanya kuwa mmoja kati ya washambuliaji waliokuwa wanaongoza kwa magoli mengi, hii ndiyo sababu kubwa iliyompelekea kocha wa Taifa kipindi kile Salum Mayanga kumwita kwenye kikosi cha timu ya Taifa kwa mara ya kwanza.
Nyota yake iliendelea kung`aa hadi kipindi cha usajili ambapo timu zote kubwa tatu za Azam, Simba na Yanga zilikuwa zikimuhitaji hali iliyowafanya Azam kumsajili na hakusita kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Azam cha kocha Cioaba mapema msimu ulivyoanza kabla ya kupatwa na majeraha ambayo kwa kiasi fulani yamemrudisha nyuma sana.
Kwa sasa siyo chaguo la kwanza la Pluijm inawezekana aina ya uchezaji wake hakujamridhisha kocha na wenzake.

HARUNA CHANONGO - MTIBWA SUGAR
Unaweza kujiuliza yule kijana fundi aliyekuwa akiitwa kwenye vikosi vya timu ya Taifa kadhaa vilivyopita yupo wapi! Yule Chanongo halisi ambaye huko nyuma akifanikiwa kuzichezea timu za Simba, Stand Utd na sasa yupo Mtibwa kwa mafanikio makubwa kiasi yupo wapi na shughuli zake ndani ya uwanja.
Chanongo yupo Mtibwa akiwa chini ya kocha Zuberi Katwila, aliwika sana ingawa hakuwa bahati ya kucheza nje kama alivyokuwa akitamani. Leo Chanongo si chaguo la kwanza la Katwila kwani anahitaji kuongeza bidii na kujishusha kwa makocha wake ili aweze fanikiwa.

MZAMIRU YASIN - SIMBA
Huyu ndiye aliyekuwa injini ya timu ya Simba kipindi cha Omog na kumalizikia kwa Lechantre  huku akionekana kama mchezaji kiraka wa namba zote.
Akiwa Mtibwa Sugar,  Mzamiru aliitwa kwenye kikosi cha Stars iliyokuwa chini ya kocha Salum Mayanga na kushiriki michuano ya Cosafa nchini Afrika Kusini, hilo pamoja na kiwango chake ndivyo vilivyowavuta Simba hadi kumsajili misimu miwili nyuma, nyuma alicheza karibuni michezo yote chini ya makocha Omog na Lechantre .
Mambo yamekuwa tofauti sana chini ya Aussems ambaye binafsi anamuona Mzamiru kama kiungo asiyekamilika na hivyo kutompa hata nafasi ya kuanza, Mzamiru ana nafasi finyu sana ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza nafasi aliyokuwa akicheza ina watu zaidi ya wanne si kazi rahisi kwake hasa unapokosa kuaminiwa na Kocha Mkuu.

EMANUEL MARTIN - YANGA
Alisajiliwa chini ya makocha Pluijm na Juma Mwambusi baada ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa kirafiki baina ya Yanga na JKU huku baada ya kuwafunga Yanga goli mbili pekee yake.  Ujio wake ndani ya Yanga ulimaanisha kupigania namba mbele ya wachezaji wazoefu kama Simon Msuva na Deus Kaseke waliokuwa wakicheza pembeni.
Baada ya kuondoka Pluijm ilionekana wazi sasa ujio wa Lwandamina kuwa neema kwake na akaanza kuaminiwa kupangwa kikosi cha kwanza kila mchezo waliocheza na alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliokuwa na magoli mengi ndani ya Yanga msimu uliopita zaidi ya goli nne na kuisaidia Yanga angalau kufikia walipomalizia.
Kwasasa maisha yamekuwa magumu sana ndani ya kikosi cha Yanga anashindwa kupata namba ya kudumu au hata ya kuanza kwenye michezo waliokwisha cheza hadi sasa, chini ya Zahera, Martin anahangaika sana na huenda akawa mmoja wa wachezaji watakaoachwa.

SALIMU MBONDE - SIMBA
Mlinzi huyu aliyesajiliwa kutoka Mtibwa msimu uliopita akiingia ndani ya kikosi na wachezaji wengi nyota kama Emanuel Okwi, Aishi Manula, Erasto Nyoni na wengineo waliokuja kuunda ukuta mzuri kwa Simba na kuisaidia klabu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi kuu kwa mara nyingine baada ya kuukosa kwa muda mrefu. Mbonde aliitwa mara kadhaa Taifa Stars chini ya makocha Charles Mkwasa na Salum Mayanga.
Msimu huu Mbonde haonekani uwanjani kutokana na kuandamwa na majeraha ya muda mrefu huku pia akiwa na kibarua kigumu cha kuwanyang`anya namba walinzi wanaopokezana sasa Juuko Murshid, Pascal Wawa na Nyoni huku kocha mzungu akiweka akili yake kubwa kwa wachezaji aliowaamini .

PAUL BUSWITA - YANGA
Mmoja wa wachezaji waliogonga vichwa vya habari kwenye dirisha la usajili wa msimu mpya wa 2017/2018 baada ya kuonekana akitakiwa na klabu zote kubwa nchini huku Simba wakitanguliza kishika uchumba cha Sg 10 milioni kisha Yanga wakaja kumsajili na kulazimika kuilipa Simba pesa yao.
Alikuwa chaguo la kwanza kila mechi kwa Lwandamina kwa muda mrefu huku ikiwa nadra sana kutokumuona uwanjani.
Ujio wa Zahera kumemaanisha kuondoka kuonekana kwenye kikosi cha kwanza kila mara hadi sasa kucheza kwenye michezo ya kirafiki tu, Yanga iliyocheza michezo tisa hadi sasa hana nafasi ya yeye kuanza hata mchezo mmoja hii ni habari mbaya kwake na kuhitaji kujitathmini.