Azam yajisalimisha mechi za Simba, Yanga

Muktasari:

Uongozi wa Azam FC umeamua kurudisha mechi zao Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wakiwa wanacheza na Simba na Yanga wakiwa kama wenyeji na sio kutumia uwanja wao wa Chamazi Complex.

MASHABIKI wa Simba na Yanga sasa washindwe baada ya uongozi wa Azam FC kuomba mechi ambazo walikuwa wenyeji zichezwe Uwanja wa Taifa badala ya Chamazi Complex.
Uongozi wa Azam FC kupitia kwa Afisa mtendaji mkuu  Abdulkarim Mohamedamin Nurdin, alithibitisha hilo kwamba waliiona changamoto msimu 2017/18 ambapo walitumia uwanja wao wa nyumbani ambapo ilikuwa ngumu kuingiza mashabiki wote.
Uwanja wa Chamazi Compelex unaingiza zaidi ya mashabiki 7,000 mpaka 10,000 wakati Uwanja wa Taifa wanaingia mashabiki 60,000.
"Tumeandika barua TFF ili kuomba tunapocheza na Simba na Yanga hasa sisi tukiwa wenyeji, tuchezee Uwanja wa Taifa, tuliiona changamoto hiyo msimu wa 2017/18 namna ambavyo timu hizo zilivyokuwa na mashabiki wengi,"anasema.