Azam yawarejesha mechi za Simba, Yanga Uwanja wa Taifa

Muktasari:

Licha ya Azam msimu uliopita kuomba kucheza mechi zao za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga katika uwanja wao wa Chamazi Complex, wameandika barua kwa bodi ya ligi kuomba mechi hizo kurejeshwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Dar es Salaam. Klabu ya Azam imeomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iwe inatumia Uwanja wa Taifa kwa michezo yake ya nyumbani dhidi ya Simba na Yanga badala ya ule wa Azam Complex Chamazi kama ilivyokuwa awali.

Kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Mohamedamin Nurdin, waliandika barua ya kuomba kurejeshwa kwa mechi zao za nyumbani kwa Afisa mtendaji mkuu wa bodi ya Ligi ili waweze kushugulikiwa suala lao.

Katika barua hiyo ilieleza sababu kubwa ya kuomba kurejesha michezo hiyo uwanja wa Taifa ni uwezo mdogo wa kuingia mashabiki na watazamaji kwenye uwanja wa Chamazi.

Barua hiyo ilieleza zaidi kwamba Msimu uliopita wa 2017/18 zilichezwa mechi mbili za Azam fc vs Simba na Azam vs Yanga, Uongozi wa klabu hiyo uliona changamoto kubwa iliyotokea kutokana na idadi kubwa ya watazamaji kukosa fursa ya kutazama mechi hizo.