Maguli afungukia namna alivyochomoka AS Kigali

Muktasari:

Mshambuliaji Elius Maguli baada ya kusaini mkataba na KMC amewashtua wapenzi wengi wa soka nchini.

Kurejea kwa Straika Elius Maguli nchini umewashtua wadau wengi baada ya kuona mchezaji huyo kama ameanza kupotea katika ramani ya soka kwani alitoka kwenda nje ya nchi na kurejea kitu ambacho sio cha kutegemewa.

Nyota huyu ambaye aliwahi kuichezea Ruvu Shooting, Stand Utd, Simba pamoja na timu ya Taifa, aliondoka nchini na kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Oman na alipomaliza mkataba wake alikuwa akihusishwa kutua katika moja ya klabu nchini Afrika Kusini.

Maguli amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia KMC, lakini kabla ya hapo alikuwa amesaini mkataba wa miaka miwili na timu ya As Kigali inayoshiriki Ligi Kuu nchini Rwanda.

Mwanaspoti lilimtafuta na kutaka kufahamu jinsi ambavyo ameweza kuchomoka katika mkataba huo wa miaka miwili kwenye klabu hiyo ya Rwanda, alisema makubaliano ya pande mbili ndio yaliyofanya awe huru.

“Kweli nilikuwa na mkataba wa miaka miwili na ile timu lakini baada ya mambo kuwaendeea kombo kutokana na serikali kujiweka pembeni na kuiacha timu kama timu walinambia kwamba pesa hakuna hivyo inabidi nitafute timu nikaona sawa,” alisema.

Akizungumzia kuhusu kuchagua kurejea nyumbani alisema kwa muda uliokuwepo alishindwa kufanya jambo lolote zaidi ya kuhakikisha kwamba anapata timu ya haraka.

“Nje huwezi ukapata timu haraka na wengi hawaelewi hilo jambo, kwahiyo baada ya kuzungumza na klabu yangu vizuri nikaona nimalizane na KMC ni sehemu sahihi kwangu,” alisema.

Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu kwamba mchezaji huyo kabla hajatimkia nchini Rwanda alikuwa anafanya mazoezi na KMC.